Makala

KINA CHA FIKIRA: Bahati ina sifa ya kuteleza, ikienda hairudi tena!

August 12th, 2020 2 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

BAHATI haibagui haichagui!

Bahati hutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mtu ana bahati yake. Lakini hakuna anayejua siku yake ya kuipata. Anayejua na kupanga siku ya kuteremsha bahati ni Mungu pekee! Ukiwa hujaipata bahati, tulia tu usubiri! Siku yako itafika! Mungu hana choyo!

Ingawa kila mtu ana bahati yake, lakini bahati ina siri zake. Kwanza, bahati haina ahadi wala haimwambii mtu siku ya kuja! Pili, bahati hailazimishwi ila huja tu siku yako ikifika! Tatu, bahati hupatikana mara moja tu! Ikija na ukaiachia iende, huwezi kuipata tena hata ukilia! Ukibahatika kuipata bahati, uitunze usiichezee! Na uitumie vizuri sana!

Bwana Papara aliingojea bahati yake kwa muda wa miaka mingi mpaka akakata tamaa! Akaanza kulalamika na kumlaumu Mungu akisema, “Eee! Mungu wangu! Mimi nimekosa nini? Mbona sipati bahati niwe na mali nyingi nitajirike kama watu wengine?!”

Alilia hivyo kwa miaka kumi! Halafu siku moja alipokuwa ameketi chini ya mti nyumbani kwake kwa huzuni, machozi yakimtoka machoni, mara alisikia sauti ikisema naye kutoka angani!

Bwana Papara alitega masikio akasikia sauti ikimwambia, “Bwana Papara umelia sana! Nyanyuka uende kule shambani kwako karibu na mto. Ukasimame kando ya mti mkubwa wa mpera ungojee hapo! Utamwona punda akitokea ndani ya mto! Akifika karibu nawe umshike mkia. Utajiona umebaki na mfuko uliojaa pesa nyingi kwenye mkono wako! Utakuwa tajiri kuliko matajiri wote wa hapa kaunti ya Malimoto! Amka uende!”

Baada ya kusema hayo, sauti ilitoweka hata kabla Papara hajauliza swali lolote!!

Bwana Papara aliondoka kuelekea kule shambani.

Alipofika, alisimama chini ya mpera alivyoambiwa. Zilipopita dakika kumi, punda mwenye sura mbaya ya kutisha alitokea mtoni! Bwana Papara alishtuka na kuzubaa! Kabla hajafikiria kumshika mkia, punda alipita akaenda! Papara alibaki akilia na kuomba punda mwingine atokee amshike mkia! Baada ya dakika kumi nyingine, alitokea punda mwenye sura ya kutisha kuliko wa kwanza!

Papara alipokuwa bado ameshangaa, punda alipita akaenda! Papara alilia na kujiangusha chini akaomba apate nafasi ya mwisho punda atokee!

Akaapa, “Sasa akija punda yeyote lazima nimshike mkia!”

Mara punda wa tatu akaja! Pale pale Papara alimrukia amshike mkia! Lakini alishtuka kuona kwamba punda huyo hakuwa na mkia!! Punda bila mkia!!

Ndugu wapenzi, hivyo ndivyo bahati inavyokuja na kupita! Wewe usipokuwa macho kuishika bahati yako, huwezi kuipata! Itakupita tu! Na bahati ikipita hairudi wala haipatikani tena! Ukibahatika kuipata bahati uitunze, usiichezee! Haitarudi tena!!