Makala

KINA CHA FIKIRA: Baraza la Kiswahili nchini litatuchokonoa kuwaenzi wafia lugha

January 22nd, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

WIKI hii namkumbuka mbunge wa zamani wa Runyenjes, Njeru Kathangu.

Kwa kizazi kipya cha vijana nchini Kenya huenda hili jina lisiwe na mashiko yoyote.

Ni sawa na majina yaliyosahaulika kama vile Naftali Temu, Henry Rono, Ben Jipcho, Elizabeth Onyambu na wanariadha wengine waliotifua vumbi katika mashindano ya riadha ya kimataifa zama zile.

Ila Njeru Kathangu hakuwa mwanariadha maarufu kama ninaikumbuka historia yake vizuri. Kathangu ni mwanasiasa ambaye awali alikuwa katika jeshi. Kwa kweli yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kujipa msimbo “Mtumishi” kabla ya kundi wa machale lililovuma kwenye Churchill Live. Almuradi Kathangu alijiita Mtumishi Kathangu.

Naye alikuwa mstari wa mbele katika kukitetea Kiswahili katika miaka ya 1990 kabla ya Katiba ya Kenya kukitambua rasmi kuwa lugha rasmi sambamba na Kiingereza.

Leo, Kathangu ambaye nina hakika bado yu hai, anazikwa angali hai kwenye kaburi la sahau. Nafikiri Kathangu alikeketeka maini wakati wa kuzinduliwa kwa tafsiri ya kanuni za bunge kwa Kiswahili mwisho mwisho wa mwaka uliopita wakati kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale na wengine walipokifanyia dharau Kiswahili.

Siku zote alipokuwa bunge, Kathangu alikuwa akizungumza Kiswahili, japo hakuwa mzawa wa Uswahilini. Kwa mpenzi wa Kiswahili kama Kathangu, ni jambo la kushangaza na kusikitisha sana kuona wabunge wakikikejeli Kiswahili na kufurahia ukosefu wao wa umilisi wa lugha hii ya taifa na rasmi. Watu wanachekea kitu kinachopaswa kuliza na kuliliwa. Aidha ilikuwaje kanuni za bunge kutafsiriwa na Watanzania?

Hilo linatuleta kwenye suala zima la jukumu la bunge katika kukiendeleza Kiswahili. Bunge lina wajibu wa kuhakikisha serikali kuu inatekeleza majukumu yake yanayohusiana na Kiswahili, lugha yenye hadhi kubwa kuliko zote kikatiba. Wabunge wanapaswa kuuliza serikali kama imetekeleza vipengele vyote vya Katiba vinavyohusiana na lugha hii ambayo mbali na kuwa chombo cha mawasiliano nchini, pia ni gundi inayowaunganisha watu wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha wabunge wanapaswa kukisema Kiswahili, hata Kiswahili kibaya bungeni, ili kuwaonesha Wakenya wengine kwamba lugha hii ni muhimu katika utambulisho wa kitaifa. Ni dhahiri kwamba wanapotafuta kura wanasiasa hasa wanaowania urais, hawana budi kutumia Kiswahili, kibaya na kizuri, kujipigia debe na kunadi sera.

Isitoshe, wabunge wa Kenya wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaunga mkono na kupitisha mswada wa kupendekezwa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa la Kenya (BAKIKE) litakaoshirikiana na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) na asasi nyinginezo kukiendeleza Kiswahili.

Na wajibu wa kuchangia kuundwa baraza la Kiswahili hautoshi; ipo haja kwa bunge kupitisha bajeti itakayowezesha baraza hilo kutekeleza majukumu yake kila mwaka wa bajeti ya serikali.

Ipo haja kuchapusha mchakato miongoni mwa wadau wote, wakiwemo wataalamu na waliowajibishwa kusawidi mswada wa kuundwa baraza. Hiyo ni njia ya pekee ya kuwaenzi watetezi wa awali wa Kiswahili kama Mtumishi Njeru Kathangu.