Makala

KINA CHA FIKIRA: Chipukizi wenye raghba ya kuandika wajihimu kuyajua mengi kuhusu fani ya uandishi

November 13th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

BAADA ya kutoka kituo cha habari cha Nation Centre katika barabara ya Kimathi jijini Nairobi miaka miwili iliyopita, nilifikiri kwamba simu yangu itaacha kuita. Lakini simu ziliendelea kunijia hata baada ya baadhi ya watu kujua fika kwamba sikuwa tena katika Jumba la Nation Centre.

Baadhi yao walikuwa wananipigia simu na kuniuliza hali katika Jumba hilo. Je, kulikuwa kwema huko katika mojawapo majumba maarufu ya habari katika eneo zima la Afrika Mashariki?

Mpaka leo sielewi kama wapiga simu walikuwa wanataka kwa dhati kunijulia hali au kuijua hali ya jumba hilo nilikowahi kufanya kazi angalau katika vipindi viwili tofauti.

Lakini simu ambazo zinaita mpaka leo na kunishangaza ni za chipukizi wanaotaka ushauri kuhusu uandishi. Hazijawahi kutindika na kupungua simu hizi. Kile ambacho sina habari mpaka leo ni wapi wanakozipata nambari zangu za simu watu hawa. Ilivyo ni kwamba kila uchao hupigiwa simu na waandishi chipukizi wanaouliza maswali kama vile kuchapisha kunagharimu pesa ngapi? Je, unaweza kunisomea mswada wangu kabla haujachapishwa? Je, utaniandikia dibaji au utangulizi au maandishi kwenye blabu katika kitabu changu? Na sijui mbona chipukizi hawa hunitafuta mimi kuwashauri kuhusu michakato ya uchapishaji? Kwa kweli sijui.

Acha nikupe mfano, mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili amenipigia simu mchana wa Jumatatu kunitaarifu kwamba ameandika “riwaya” ya kurasa 20 zilizopigwa taipu au kwa maandishi ya mkono daftarini kurasa thelathini. Hilo mimi lilinifanya kuhisi nimefarijika sana.

Ninakumbuka kwamba nimeanza mwenyewe kujaribisha maandishi ya kitabu changu cha kwanza nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili. Shule yangu ya sekondari nilikosomea ilikuwa na mhazili mmoja mwanamume aliyenionea imani akaichapa kazi yangu kwa taipureta yake. Hicho ndicho kitabu changu nilicholimbuka kukiandika na ambacho kama kwa mwanafunzi huyu wa shule ya Maranda, kilikuwa na kurasa chache kabisa.

Nilifurahi kusema na mwanafunzi huyo na kumhamasisha na kumshajiisha. Ni matumaini yangu kwamba alichochewa na kauli yangu kwamba tumeanza kuandika katika kidato kile kile; sote tumeanzia kidato cha pili. Kwa kweli katika pitapita zangu katika shule mbalimbali nchini Kenya, nimekutana na vijana wengi wanaoonesha azma ya kuwa waandishi; nalo ni jambo la kutumainisha sana. Wengi wao hawana habari kuhusu mchakato wa kuanzia kutunga mswada hadi kuwa na kitabu kinachouzwa madukani.

Mara nyingine hata walimu wenye azma ya kuandika nao pia wanatatizika wafanye nini kuchapisha au kuchapishiwa kazi zao. Wanafikiri, kama wanafunzi wao, kwamba mwandishi sharti awe na pesa ndiposa achapishiwe.

Mwalimu mmoja anayeyavulia nguo maji ya kuandika aliniomba majuzi yale hela za kuchapishiwa kwa msingi wa jambo hilo. Nilipomwambia kwamba sikuzote naandika miye na wachapishaji ndio wanaotumia hela zao nyingi kusoma, kuhariri, kuruwaza, kuchapisha, kuuza, na kusambaza vitabu vyangu, alishangaa ghaya ya kushangaa.

Kwa waandishi chipukizi wote nakuambieni waulize wajuao na msikate tamaa.