Makala

KINA CHA FIKIRA: Hadhari mno ahadi za serikali kuhusu Baraza la Kiswahili

September 25th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

WATU wenye matumaini wanapenda kutumaini pawepo au pasiwepo msingi wa kutumaini.

Hawataki kuitwa wendaguu, yaani watu wasiokuwa na matumaini.

Ndivyo walivyo wafurukutwa wengi wa Kiswahili. Wakiona dalili ndogo ya maendeleo ya Kiswahili wanashangilia kana kwamba Mo’ Salah kafunga bao.

Kwao dalili ya mvua si mawingu, hata baridi ni dalili ya mvua, hata joto pia.

Ndiyo maana nimewaona wakishangilia sana pendekezo la baraza la mawaziri Uganda kuidhinisha kuundwa kwa Baraza la Kiswahili.

Mitandao na majukwaa ya kijamii yalijaa pomoni kongole kwa Uganda kwa hatua hiyo muhimu katika kukiendeleza Kiswahili.

Ni tamko la serikali lenye kuwapa matumaini wakereketwa wanaotamani siku zote Kiswahili kiwe juu kama zilivyo lugha nyingine za dunia; si Kiingereza si Kifaransa, si Kireno, si Kijerumani si Kichina.

Hata hivyo, katika nyoyo za maafisa wa serikali wa Uganda, Kiswahili bado ni lugha ya kigeni isiyokuwa na tija. Tishio kwa Kiganda hasa. Waishia katika matamko matupu, hakuna utekelezaji wa maana.

Hii si mara ya kwanza kwa matamko ya kutamanisha kutajwa Uganda, Kenya, Tanzania na Rwanda; matamko matupu yasiyokuwa na dhati ya utendaji.

Maneno matupu

Viongozi wanapenda maneno matupu.

Tazama kwa mfano tamko la Tanzania mnamo 2015 kwamba Kiswahili kitatumiwa kuwa lugha ya kufundishia hadi chuo kikuu na liwe liwalo. Yalikuwa maneno matupu.

Hakuna nia kwa serikali ya Tanzania kulitekeleza hilo. Wanafunzi wa Kitanzania bado wanafundishwa kwa Kiingereza wasichokifahamu fika tokea sekondari hadi vyuo vya kati na vyuo vikuu. Wanafundishwa kwa Kiingereza na walimu wasiokifahamu fika Kiingereza.

Rwanda ilitangaza kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi za nchi hiyo mbali na Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa. Lakini wanafundisha Kiswahili kama somo la hiari katika kiwango cha chini cha sekondari tu. Yaani mwanafunzi hakutani na Kiswahili ila pale anapoingia na kukichagua kuwa somo katika kiwango cha chini cha sekondari. Anakumbana nacho kama lugha ngeni, lugha ajinabi kabisa. Ipo pembeni mno katika utendaji ingawa inaonekana kuwa mbele ikiwa unatazama tu matamko ya ajabu ajabu ya serikali.

Uganda ina tatizo baya zaidi. Si tu kwamba kuna kasumba kwamba Kiswahili ni lugha ya ukatili wa wanajeshi wa Idi Amin ‘Dada’ bali ina ushabiki mdogo sana katika umma na uongozi wa nchi.

Katika masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki si aghalabu kumsikia mwakilishi wa Uganda akizungumza Kiswahili kwa hiari.

Isitoshe, kama Rwanda, Uganda inatoa fursa ya kujifunza Kiswahili kama somo la hiari sekondari. Hakifundishwi katika shule za msingi. Mwanafunzi anakumbana nacho baadaye katika safari yake ya masomo, kikiwa lugha ajinabi kabisa ambayo tija yake haijulikani.