Makala

KINA CHA FIKIRA: Heri adui mwerevu kuliko rafiki mwovu

July 15th, 2020 2 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

KADANDIE alikuwa rafiki yangu.

Nasema alikuwa rafiki yangu kwa sababu hivi sasa siye rafiki yangu tena. Nimemkataa! Heri nikae peke yangu kuliko urafiki na Kadandie.

Mimi na Kadandie tunasoma katika darasa moja shuleni Kambikambo. Ningekuwa na uwezo ningehama nitoke katika darasa letu hili la pamoja na Kadandie. Lakini sina uwezo kiasi hicho! Siwezi kuyafanya mambo ambayo ni zaidi ya uwezo wangu.

Hapo mwanzo mimi na Kadandie tulipendana sana. Tusingetengana kwa dakika tano bila kuonana. Lakini baadaye, mimi Kachuji mwana wa Paki, niligundua kwamba rafiki mbaya ni hatari kuliko nyoka!

Leo ninaamini kwamba afadhali kukaa na adui mwerevu kuliko rafiki mjinga mwovu! Rafiki mwizi, mlevi na mvuta bangi ni hatari zaidi! Akiiba, watu husema nyinyi nyote mliiba pamoja! Akilewa na kuvuta bangi zake, na wewe watu hupita karibu wakikunusanusa kuthibitisha kama kweli hunuki bangi au pombe! Mtembea na muuza shombo hunuka shombo!

Kadandie hakuwa akisoma! Kila kazi alitaka nimfanyie mimi. Majibu ya maswali ya mtihani alizoea kuyanakili kutoka kwangu! Tukipewa kazi ya ziada tukafanyie nyumbani, Kadandie alinipa daftari lake nikamfanyie kazi yake ya ziada na kumjibia maswali! Kisha hunipumbaza kwa kunipa pesa kidogo, peremende, maandazi, biskuti na vijitakataka vingine ambavyo vyote nilivikataa! Samaki aliyepanua mdomo ndiye anayekamatwa kwa chambo! Samaki aliyefumba mdomo chambo kitapitia wapi? Nilikataa kupanua mdomo ili nizuie chambo cha ndoano ya Kadandie. Na wewe je? Ukimwona mamba amelala kapanua kinywa usidhani anacheka! Ametega mtego! Kiumbe kikiingia tu kinywani, hubanwa na kugeuzwa kuwa kitoweo!

Mwanzo mwanzo huko nilimsaidia sana Kadandie. Nilidhani angeamka na kutia bidii! Kumbe aliyeonja asali huchonga mzinga! Nilipogundua kuwa Kadandie habadiliki wala hataki kuamsha ubongo wake, nilimkataa na kuuvunja urafiki wetu ili ajitahidi kujitegemea asonge mbele kwa bidii zake.

Ni vizuri mtu kujikaza na kujifanyia kazi!

Simtaki tena rafiki mzembe, mlevi, mwizi anayeiba vitu vidogo vidogo vya wazazi wake kuniletea rushwa au hongo za kunipumbaza akili ili nimfanyie kazi zake kwa raha zake huku akinitumia kama bwege! Hapana!!

Katika maisha usipoerevuka na kujanjaruka mapema kama Kachuji mwana wa Paki na kuwaepuka akina Kadandie, utatumiwa vibaya ujute! Hatari kwa maisha yako.

Uwachunguze sana rafiki zako uwajue tabia zao na nia zao katika uhusiano wenu! Usikubali kusukumwa tu kama mkokoteni au toroli kuenda kufanya matendo mabaya kana kwamba huna akili! Hao wanaokusukuma si marafiki wema!

Heri ukae na adui mwerevu kuliko kukaa na rafiki mjinga mwovu! Erevuka!!