Makala

KINA CHA FIKIRA: Japo safari bado ndefu, ni hatua nzuri kwa SADC kupaisha Kiswahili Afrika

August 21st, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

MAPEMA Machi 2019 nilialikwa kutoa mada elekezi katika kongomano la wanahabari wanaotumia Kiswahili.

Mwenyeji wangu Prof Aldin Mutembei kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alinipokea kwa moyo mkunjufu.

Niliwahi kusimulia katika safu hii jinsi alivyonipeleka kufikia kwenye hoteli moja uchwara huko Sinza iitwayo Fahari.

Sikukuambia kuhusu mafuriko yaliyokuwa yamekithiri Sinza wakati huo na kutufanya sote waendao kwa miguu kukanyaga kwenye vidimbwi vya maji yaliyotufikia magotini.

Na hayo ya kupelekwa Fahari Hotel kule Sinza nilikuwa nayasema kwa utani kwa vile shughuli muhimu haikuwa wapi kanipeleka Prof Mutembei kufikia.

Aidha sikukuelezea kuhusu jinsi mambo yalivyokuwa katika ofisi ya Prof Mutembei. Prof Mutembei alinipokea kwa mawili na matatu, ila alikuwa kakumbwa na kukurukakara chungu mbovu.

Nilipothubutu kumuuliza aliniambia alikuwa anashughulikia mapendekezo muhimu kwa ajili ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kulikuwa na stakabadhi muhimu sana aliyokuwa anaipiga msasa kabla kuiwasilisha kwa viongozi wakuu wa shirika la SADC.

Naam kwa kweli alinidokezea kwamba stakabadhi hiyo ilikuwa sehemu ya mikakati ya kuijumuisha lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa hiyo tangazo la wiki jana kwamba Kiswahili kimeongezwa katika lugha rasmi za Jumuiya ya SADC ni tukio la furaha na fahari kwangu.

Hivyo ndivyo ilivyo hasa kutokana na ukweli kwamba nilishatagusana na majemedari wa Kiswahili kama Prof Mutembei waliochagua Kiswahili kupanda chati kama vile ambavyo baadhi ya wakereketwa wameelezea mafanikio haya.

Gazeti la Uhuru linalochapishwa lilibeba kichwa cha habari ‘SADC yapaisha Kiswahili Afrika’.

Katika Jumuiya ya SADC lugha rasmi zimekuwa Kireno, Kifaransa na Kiingereza. Hapana shaka kwa kweli Kiswahili kimekwezwa au kimepaishwa kama linavyosema gazeti hilo la Tanzania.

Sina shaka kwamba wapo wengi waliochangia kimya kimya kukipigia upatu Kiswahili katika SADC bila wao kuonekana wala kusikika.

Inawezekana kwamba mathalani Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) imechangia ufanifu huo vilevile, sikwambii wengi wengine wenye ghamidha ya kukiona Kiswahili kinatamba duniani. Kwa wote hawa nasema kongole kwa ufanifu wenu mkubwa.

Tunajenga nyumba moja tusipiganie fito.

Pamoja na matangazo haya yenye kutia moyo, sharti tukiri kwamba safari ya Kiswahili bado ndefu; bado hakijakaribia nchi ya ahadi.

Tazama kwa mfano ukweli kwamba si mataifa yote ya Afrika Mashariki, chimbuko la Kiswahili, ni wanachama wa Jumuiya ya SADC.

Tanzania ndiyo nchi ya pekee ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo mwanachama wa SADC.

Ni heshima kubwa kwa nchini nyingine 13 wanachama kuridhia kutumia lugha isiyotumika kwao kuwa lugha rasmi.

Je, Tanzania pekee yake itatosha kuzifanya nchi hizi nyingine kuzungumza Kiswahili kwa mapema na marefu.

Je, tutashangiliaje SADC kukipaisha Kiswahili ilhali zaidi ya mwongo baada ya AU kukipaisha hakuna mjumbe wa Afrika Mashariki anayokitumia kwenye vikao? Hatujengi ghorofa kwa karata hapa?