KINA CHA FIKIRA: Jifunge masombo utafute mali yako ufurahie maisha

KINA CHA FIKIRA: Jifunge masombo utafute mali yako ufurahie maisha

Na WALLAH BIN WALLAH

BIDII za mtu ndiyo mafanikio yake.

Mwenyezi Mungu akikujalia uhai na uzima, uwezo na nguvu, akili na maarifa, basi uvitumie vipawa hivyo kujitafutia riziki maishani. Ndipo wataalam waliposema, “Tumia karama uliyo nayo ili upate usichokuwa nacho!” Nao wahenga wakaongezea kwamba, “Mtegemea cha nduguye hufa maskini!” Jitahidi sana utafute mali yako kwa jasho lako utumie badala ya kutegemea mali ya nduguyo!

Yumbayumba na Sombasomba na Songasonga walikuwa watoto wa kiume wa Bwana Kazamoyo. Baba yao aliaga dunia baada ya kuketi nao chini na kuwapa mawaidha na wosia kwamba, “Wanangu, duniani hapa pana kila kitu ambacho mwanadamu anahitaji katika maisha yake! Mtu akifanya bidii kwa nia thabiti, hawezi kukosa njia ya kujipatia mahitaji yake muhimu maishani!” Akakata roho! Wanawe walibaki peke yao watu wazima wenye akili zao, nguvu zao na elimu vichwani. Yumbayumba mvulana kifunguamimba, wa pili Sombasomba na Songasonga mvulana kitindamimba!

Sombasomba alifanya kazi zake kwa bidii kama mchwa! Licha ya elimu yake kichwani, alianza kwa kuwabebea watu mizigo mizito kutoka mashambani kupeleka sokoni. Akajifunza faida ya kusomba mizigo ya bidhaa kupeleka sokoni. Akaanza biashara zake mwenyewe. Baada ya miaka kumi alitajirika akajenga jumba kubwa zuri la kuishi kwenye shamba lile lile dogo waliloachiwa na marehemu baba yao! Akaishi vizuri huku akiendelea kufanya biashara zake. Lakini ndugu zake Yumbayumba na Songasonga walikuwa wavivu na wazembe wasiopenda kufanya kazi yoyote! Walipopata pesa zao walizitumia katika starehe na anasa za dunia! Wakaishi maisha ya uchochole na umaskini bila mbele wala nyuma! Kila mara walienda kuomba misaada ya chakula, mavazi na pesa kutoka kwa ndugu yao Sombasomba! Hatimaye wakawa wanyonyaji kama kupe wa kumtegemea Sombasomba kwa kila kitu mpaka wakatamani Sombasomba aage dunia ili warithi mali yake!

Baada ya miaka mingi, wote watatu wakawa na umri mkubwa! Sombasomba aliamua kuhama aende kuishi mbali na ndugu zake. Siku moja aliwaketisha chini akawambia, “Mimi ninahama! Lakini nawaachia nyumba yangu nzuri na utajiri wangu wote chini ya nyumba hii! Mkichimba mtapata pesa zangu zote zimo chini ya nyumba hii!!” Akaondoka.

Sombasomba alipoondoka tu, ndugu zake walianza kuchimba kuzunguka nyumba ili watoe pesa zilizokuwa chini ya nyumba! Walichimba sana mpaka nyumba ikaporomoka na kuanguka chini! Hapo ndipo walipoona sanduku kubwa la chuma wakalipasua! Ndani walipata kokoto na mchanga uliofungwa kwa karatasi ngumu iliyoandikwa, “WAVIVU NYINYI!! HAMJUI KUWA MTEGEMEA CHA NDUGUYE HUFA MASKINI?? TAFUTENI MALI YENU MTUMIE!!”

Ndugu wapenzi, utajiri wako ni bidii zako! Jitahidi utafute mali yako utumie maishani!!

You can share this post!

BI TAIFA JANUARI 6, 2021

SAUTI YA MKEREKETWA: Usalama wetu na wa watoto shuleni ni...