Makala

KINA CHA FIKIRA: Kisa cha Mlajasho mfano kwa vijana

July 29th, 2020 2 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

DAWA ya umaskini ni kazi.

Umaskini utaisha tukifanya kazi kwa bidii. Katika nchi yetu, kazi ziko nyingi. Lakini wanaopenda kufanya kazi ni wachache mno!

Watu wengi hudhania ati kazi ni za kuajiriwa tu na kupokea mishahara kila mwezi!

Kazi ni shughuli yoyote unayofanya ikuletee mapato, pesa na chakula. Si lazima kila mtu aajiriwe! Unaweza kujiajiri mwenyewe ujifanyie kazi upate pesa utajirike kama wengine.

Mafanikio katika maisha huhitaji akili, bidii na uwezo wa kufanya kazi kwa kujituma. Siyo lazima mtu awe na karatasi ya kuonyesha alivyosoma kidogo au sana shuleni. Karatasi haifanyi kazi! Mtu ndiye anayefanya kazi. Anaweza kuajiriwa au kujiajiri kuwa mkulima, mfugaji, seremala, msusi, kinyozi, mfanyabiashara au kazi yoyote kulingana na akili au uwezo alio nao!

Kijijini Songambele kuna maduka madogo madogo au vibanda vinavyoitwa vioski. Huko ndiko wanakijiji wanakonunulia vitu muhimu katika maisha ya kila siku kama vile mikate, sukari, chumvi, mafuta, unga, maziwa, viberiti, sabuni na vinginevyo. Na wauzaji hujipatia pesa kwa kazi zao muhimu za kuuza bidhaa!

Kibanda au kioski kinachopendwa zaidi kijijini Songambele ni MALIMALI ambacho ni cha Bwana Keni Mlajasho! Bwana Keni Mlajasho alizoea kukifungua kioski chake mapema alfajiri saa kumi na nusu kabla ya wauzaji wengine hawajafungua.

Alifunga usiku baada ya wengine kuvifunga vioski vyao. Kwa ukweli wauzaji wengine walivifungua vibanda vyao kwenye saa mbili au tatu asubuhi na kuvifunga saa kumi na mbili au saa moja usiku!

Na walipovifungua vioski vyao saa mbili au tatu, tayari wateja waliotaka bidhaa mapema ili wajitayarishie kifunguakinywa waende kazini, watoto wao pia waende shuleni, huwa wameshanunua kutoka kwenye kioski MALIMALI kwa Bwana Keni Mlajasho. Watu wakazoea kwa Bwana Mlajasho maana alifungua mapema. Pia walipata mahitaji na bidhaa zote walizohitaji. Mlajasho akawa maarufu! Baada ya miaka kadhaa akatajirika sana!

Sasa hivi ameanza kujenga duka kubwa hapo hapo Songambele.

Majirani waliokuwa na vioski wamefilisika kutokana na uvivu, kupenda usingizi, kuchelewa kufungua, kufunga vioski mapema na kukosa kuleta bidhaa muhimu!

Juzi mwanahabari mmoja alimhoji mwenye kioski aliyekuwa jirani wa Mlajasho pale MALIMALI! Akamuuliza kwa nini alifilisika akafunga kioski chake!?

Muuzaji huyo alijibu, “Mlajasho ndiye aliyeiroga biashara yangu, ikaanguka nikafilisika!” Upuuzi mtupu huo!

Naam, leo ninaomba kumwambia huyo ndugu aliyefilisika pamoja na wazalendo wengine kwamba, “Uchawi wa kumroga mtu ni UVIVU wake mwenyewe!”

Ukifanya kazi zako vizuri kwa bidii, utafanikiwa tu!

Uvivu ni nyumba ya njaa! Dawa ya umaskini ni kazi, si uvivu! Anza leo kufanya kazi kwa bidii!! Utafanikiwa!!

[email protected]