Habari

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kilipata utanuzi mkubwa mno katika enzi ya Moi, makiwa kwa wote

February 12th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

HUU si wakati mzuri wa kufa.

Hili halitokani na hatua alizopiga mwanadamu katika kuboresha miundumbinu na teknolojia kwa jumla. Rafiki yangu mmoja, na sasa simkumbuki nani, aliniambia mwaka 2019 kwamba huu si wakati mwafaka kufa kwa vile ukifa unapitwa na uhondo wa maendeleo ya mwanadamu katika uvumbuzi na ugunduzi wa mambo tumbi nzima.

Sikubaliani naye hata sasa na sikukubaliana naye alipoyatamka aliyoyatamka. Nakubaliana naye kuhusu suala la kwamba sasa si wakati mwafaka wa kufa, ila kwa sababu yake sikubaliani naye.

Leo nasema kwamba hakuna tija ya kufa sasa hasa kutokana na kizazi hiki cha watu makauleni wanaokusifu na kukukashifu kwa pumzi moja na kinywa kimoja.

Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke Margaret Thatcher 2013 ndicho kilichonizindua kwa tabia hii ya kukirihisha. Watu walijificha nyuma ya pazia la majina bandia ya majukwaa ya mtandaoni kukomoa na kuua maiti. Walisema walivyokuwa mwovu Bi Thatcher na kwamba dunia ilikuwa afadhali bila yeye. Nilimaka sana. Katika hukumu hakuna wakali kama watu wa kizazi kilichoko. Wanajua kuhukumu kuliko Mwenyeezi Mungu, yaani machoni pao. Hakimu wa haki kama wao hakuna. Wao ndio wajuao. Nani kama wao?

Nimeona tangu kifo cha Rais wa Pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich arap Moi, mambo yamekuwa yale yale. Watu wanapozungumza hadharani kwenye runinga na mawanda rasmi, wanampalia sifa kiongozi huyo aliyetuacha mkono. Wakigeuka pahali ambapo si rasmi wanatema cheche za matusi na lawama. Wanatukana tu na kutusi kama cherehani. Na hakuna pahali ambapo hilo limebainika zaidi kama katika majukwaa yaitwayo ya kijamii mtandaoni kama Twitter, Facebook and kwengineko.

Wanasema mabaya mpaka yanakuchusha na kukuchosha. Mimi nishachoka.

Siwezi kufanya kazi ya Mwenyeezi Mungu ya kuhukumu watu. Wacha wafao wafe, na hukumu tumwachie mwenyewe Muumba. Niliwahi kuhudhuri mazishi ya Profesa mmoja maarufu sana. Yeye alikuwa miongoni mwa watu walionirai nipate kisomo cha tija.

Niliona vile waliopanda jukwaani walivyomsifu sana kwa umahiri wake wa kitaaluma na utu wake wema. Haya walikuwa wanayasema kwenye maikrofoni. Ila wakishuka toka jukwaaani wanasemezana wao wa wao kuhusu mapungukiwa au mapungufu ya marehemu. Mwone alivyokuwa hana mke, hana nyumba, kazikwa katika shamba la nduguye.

Hii ni nini hii? Wanamkosoa pakubwa mtu ambaye hayupo hapa kujitetea mwenyewe dhidi ya lawama zao.

Katika siku hii ya mazishi ya Mzee Daniel Toroitich arap Moi, sina nia ya kumsifu wala kumkashifu, kama nikikopa maneno ya Bruto katika tamthilia ya Shakespeare cha Juliasi Kaizari iliyotafsiriwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Ninachotaka kusema ni kwamba ni katika enzi yake ambapo Kiswahili kilipata utanuzi mkubwa zaidi tangu kujipatia uhuru.

Ni Mzee Moi ndiye aliyekifanya Kiswahili somo la lazima katika mfumo wa elimu.

Nasema makiwa sana kwa wote wanaohusika na msiba wa kuondokewa na Baba Moi.