Makala

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitafana iwapo wanahabari watazidisha utashi

April 29th, 2020 2 min read

Na KABRASHA LA HISTORIA

WIKI jana (Juma la kwanza Mei, 2019) katika Taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulifanyika kongamano la kihistoria. Lilikuwa kongamano la kwanza kabisa la vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili kutoka pembe zote duniani.

Mgoda wa Kigoda cha Nyerere katika taasisi hiyo Prof Aldin Mutembei alikuwa ndiye mwandalizi mkuu akisaidiwa na Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Dkt Musa Hans na wengine. Mimi nilishtuka sana Prof Mutembei aliponiomba nitoe mada elekezi ya kongamano; nilihisi kanivika joho ambalo si makamo yangu kulivaa.

Ukumbi ulikuwa umejaa hakuna pahali pa kutema mate, umejaa wan- ahabari na wanahabari watarajiwa. Nilifika nikaamka kutoa mada elekezi, nikisema, japo kwa kutetemeka. Hata hivyo, ilikuwa furaha iliyoje kuwaona wanahabari kutoka pembe mbalimbali za dunia wakishauriana kuhusu utendakazi wanapofanya kazi yao kwa kutumia lugha adhimu ya Kiswahili!

Wanahabari hawa waliungamanishwa si tu na taaluma yao bali na Kiswahili kama wenzo wao wa utendakazi. Tulijadili mengi kuhusu hali ya awali, ya sasa na ya baadaye ya Kiswahili katika vyombo vya habari. Tulijaribu kujibu swali Kiswahili kilikuwaje, kikoje, na kitawakuwaje katika mustakabali wake. Midahalo ilikuwa wazi nyeti na yenye ucheshi sawia. Aghalabu kila mtu katika hadhira alivutiwa na hotuba kama ile ya Austere Malivika kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyesimulia kwa kina kuhusu kuripoti kutoka uwanja wa vita. Aliwashtua wengi kwa ujasiri wake wa kutafuta habari katika mazingira hatari sana ambapo mpaka uliopo kati ya kufa na kuishi ni mdogo kabisa.

Naye Kauthar, mwanamke mzawa wa Pemba aliwazuzua watu kwa utetezi wake wa wanawake wanahabari. Aliuponda sana mfumo wa ubabedume ulioshamiri hata katika vyombo ambavyo vinatumia Kiswahili. Labda sasa unajiuliza nami nilitoa hoja zipi katika mada yangu elekezi? Nilitaka nikuambie kwamba usafiri wangu wa kuenda Dar ulikorofisha – nikaachwa na ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta. Kisa na maana, sikusoma vizuri tiketi yangu na wakati ndege yangu ingeondoka, nilikuwa Huduma Centre, Nairobi nin-

afuatia Namba yangu ya Huduma. Ila sasa utasema na hilo linahusu nini kongamano? Kwa hiyo acha nikupe muhtasri wa hotuba yangu.

Mada yangu ilikuwa “Tafakuri kuhusu mustakabali wa Kiswahili katika vyombo vya habari.” Kwa kuchelewa kufika niliitoa Jumamosi badala ya Ijumaa. Ila muhimu ni kwamba nilisisitiza kwamba Kiswahili kitafana tu endapo wanahabari watakuwa na utashi wa kukiendeleza, wanahabari waliosimama kidete kukifia Kiswahili.

Nilitoa mifano ya mikota wa zamani wa tasnia hii ya uanahabari kama vile Salim Mbonde, Sera Ndumba, Abdul Ngalawa, Leonard Mambo Mbotela, Daniel Njuguna Gatei na Elizabeth Obege ambao walijitolea kusarifu lugha kwa ufasaha. Nilikosoa tabia za watangazaji kupachapika ovyovyo maneno ya Kiingereza kama mtangazaji aliyesema nikiwa Dar: “Kipa Manulla ana-doubt marking ya Mohamed Hussein. Naam, baadhi ya wanahabari lao kubwa ni kukiua Kiswahili.

TANBIHI: Hii ni kumbukumbu mojawapo ya kauli ya marehemu Ken Walibora