KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitukuzwe kwa vitendo badala ya maneno matupu

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitukuzwe kwa vitendo badala ya maneno matupu

Na WALLAH BIN WALLAH

KATIKA kitabu maarufu cha riwaya kiitwacho Nyota Ya Rehema alichokiandika mwanafasihi mahiri wa Zanzibar, Bwana Mohamed Suleiman Mohamed, kikachapishwa mwaka 1976, mwandishi anabainisha mgogoro kati ya Bibi Adila na Bwana Fuad kuhusu Bi Aziza!

Adila amwambia Fuad, “Ha-a-a! Unakaa na mtu usiyemtaka kumwudhi unayemtaka…….ati kwa sababu unaona huruma! Basi fanya uchague; unayempenda bila ya huruma au unayemhurumia bila ya kumpenda……..!”

Kwa mintarafu ya kauli ya Bibi Adila, ninaomba nisuke kauli kuwaambia wanasiasa, wanasheria wasomi na viongozi wetu kwamba, ‘Ha-a-a! Mnaisifia lugha ya Kiswahili msiyotaka kuitumia wala kuizungumza ili kuwafumba macho wazalendo wapigakura ati kwa sababu mnawaonea huruma za mamba!

Basi fanyeni kuchagua kimombo mnachokipenda bila ya kujidai mna huruma, au mtumie Kiswahili cha wazalendo mnaojidai kuwahurumia bila ya kukipenda Kiswahili lugha yao…….!’Sisi sote tunajua fika kwamba viongozi wetu wasomi, wanasiasa pamoja na wanasheria walisimama kidete kutetea Kiswahili kuwekwa kwenye Katiba kuwa lugha rasmi ya taifa letu.

Kiingereza ikawa lugha ya pili rasmi nchini. Katika juhudi kubwa za kutimiza azma ya kutambua umuhimu wa Kiswahili, bunge la taifa liliidhinisha kuundwa Baraza la Kiswahili nchini! Nani asiyejua hayo?Kichekesho na kejeli ni kwamba licha ya viongozi wetu kukitetea Kiswahili hadi kukisukumiza katika Katiba kuwa lugha ya taifa, wao wenyewe hawakitumii wala hawajivunii Kiswahili!!

Popote wanapozungumza vikaoni, mikutanoni, hadharani, ofisini au bungeni; wanakumbatia na kung’ang’ania ung’eng’e wao au kimombo chao tu!

Aghalabu utawasikia wakijisifia na kusifia ati Kiswahili ndiyo lugha ya taifa; ni umoja wetu; lakini huwaje wanasifia kwa maneno matupu bila ya vitendo katika mikakati na harakati zao za kitaifa?

Marehemu Babu yangu aliniambia, “Ni salama zaidi endapo mtu anakudanganya ilhali unajua anakudanganya! Lakini ni hatari zaidi kudanganywa bila ya kujua kuwa unadanganywa!”

Nyote mnakumbuka juzi juzi Ijumaa tarehe ishirini wanasheria majaji wasomi wa mahakama ya rufaa walipokuwa wakitoa uamuzi kuhusu mchakato wa maridhiano (BBI), walisema ati, ‘Moja kati ya sababu za kukatalia mbali mapendekezo ya maridhiano hayo ni kwamba matumizi ya lugha ya Kiswahili hayakuzingatiwa!! Kinyume cha mambo!

Wao wenyewe walikaa wakasoma uamuzi wao na hukumu zao kwa muda wa saa kumi bila kutamka hata neno moja la Kiswahili!

Waliipuuza lugha rasmi ya taifa wakakoroga kimombo chao mpaka mwisho, kisha walijidai na kudai Kiswahili hakikupewa kipaumbele!

Ndugu wapenzi, tujitokeze na tujitolee kukitukuza Kiswahili kwa vitendo badala ya kukisifia kwa maneno matupu tu! Kiswahili kitukuzwe kisipuuzwe!!!

You can share this post!

NASAHA: Ipe mipango yako ya kiakademia kipaumbele ili upate...

Hichilema aapishwa huku raia wakitarajia mwamko mpya