Makala

KINA CHA FIKIRA: Korona ya kuenzi Kiingereza inaua Kiswahili chetu

March 18th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

MARADHI ya Korona yalifika Nairobi nikiwa Nairobi.

Yamefika Dar es Salaam na Zanzibar nikiwa Pemba. Kwa hakika maradhi haya ndiyo yanagonga vichwa vya habari kila pembe duniani hata Pemba ninakoandikia makala haya.

Dunia nzima inatikiswa na homa hii isiyokuwa na tiba. Nilipopanda ndege kwenye uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, niliomba kupewa barakoa maana madukani sizioni.

Afisa mmoja wa afya akanionea imani akanipa nikavaa hii barakoa mara ya kwanza maishani. Sijawahi kuivaa barakoa inayoziba pua na midomo na kutatizika kupumua.

Niliivua kidogo, tulipopitishwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, nikaona kuduwazwa na maajabu ya maumbile ya Mwenyezi Mungu.

Ndege ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Amaan, Zanzibar, tukalakiwa kwa kupekuliwa afya zetu kwa kidude kama bunduki. Unaelekezewa kipajini na sikioni.

Sijui kama kinapima na kudodosa maradhi ya Korona au halijoto ya mwili tu. Tukaandikishwa fomu za uangalizi, kwa maana kwamba watakufuata popote ulipo kujua hali yako. Zanzibar nayo imetikiswa ati. Ila nilipotaka kuingia sehemu ya ndege ya ndani, niwahi kuunganisha safari ya kuenda Pemba, mtu mmoja kaniambia nivue barakoa.

“Zanzibar salama,” katamka.

Je, Zanzibar salama? Zanzibar itakuwaje salama? Haidhuru nilisalimu amri nikaivua barakoa yangu na kuitumbukiza jaani. Zanzibar salama! Zanzibar salama vipi?

Niliwasili Pemba jioni kwa wenyeji wangu waliokuja uwanja wa ndege kunipokea. Pindi tulipofika nyumbani ikaja habari kwamba mgonjwa wa kwanza wa Korona kapatikana Dar es Salaam, Tanzania.

Wakati naandika makala haya hata Zanzibar yamefika. Kauli ya mtu yule kwenye uwanja wa ndege kwamba Zanzibar salama, yalikuwa maneno matupu, maneno ya kizalendo yasiyokuwa na tija, mafamba na majigambo ya watu wanaopofushwa na uzuzu.

Uongo huu ndio niliokutana nao bibi mmoja aliponiambia Nairobi wiki iliyopita kwamba Korona haiwezi kuja Afrika, kwa sababu Mungu anapenda Waafrika.

Yaani Mwenyezi Mungu anawachukia wanadamu wote na kuwapenda Waafrika tu. Jamani tuache kujidanganya na kujihadaa kwa ndoto za Alinacha.

Na haya ya Korona wala si mada halisi ya mjadala wangu leo. Ni utangulizi. Katika pitapita zangu Zanzibari nikisubiri ndege ya kunipeleka Pemba, nimeona mabango yanayosema: “Jifunze Kiingereza kwa katuni, nyimbo na picha.”

Kwangu mimi huwezi kuwa na matangazo kama haya na kisha udai kwamba u salama. Zanzibar kuwa salama ni uongo hatari hata kilugha.

Kumbe hata Zanzibar, ipo hii Korona iliyoenea Kenya na Uganda, na Naijeria na Ghana kwamba sharti tukijue Kiingereza ima fa ima.

Korona ya kukipenda Kiingereza cha mkoloni, kukienzi kama mboni ya jicho. Hii ni Korona ya kukikadiria Kiingereza kama chenye thamani kubwa kuliko lugha zetu kama vile Kiswahili. Haya ndiyo aliyoyasema Ngugi wa Thiong’o kwamba mafanikio makubwa zaidi walioyatekeleza wakoloni ni kutufanya tuchukie lugha zetu.

Kuna Korona ya lugha inayoangamiza lugha zetu, na kuna korona ya kiafya iliyotoka China.