Makala

KINA CHA FIKIRA: Kwa nini Kiswahili sanifu hakipati mwanya wa matumizi katika nafasi za umma?

March 4th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

“USIKAE tu bila job. Tutakusaidia kwenda majuu upate job.”

Hivyo ndivyo bango moja linalokingama barabara ya Gitanga kwenye eneo la Valley Arcade hapa jijini Nairobi linavyonadi.

Wapitao kwa miguu na kwa magari wanayakodolea macho maneno haya yanayotangaza ajira ughaibuni.

Hata watoto wanaosoma Kiswahili sanifu shuleni wanakumbana na Kiswahili hiki cha kona kwenye bango hilo. Ndicho Kiswahili wanachokisikia wanafunzi hawa kikisemwa redioni wakati wa vipindi vinavyozungumzia unyumba na ufuska bila vizuizi waya haya. Ndicho Kiswahili kinachosikika, kanisani, sokoni, majumbani ndani ya matatu.

Mimi nimefikia mkataa kwamba watoto wa siku hizi wanasoma na kusikilizishwa mambo wasiyopaswa kuyasikia katika Kiswahili wasichofundishwa Kiswahili.

Kwa hakika, kama wapo walimu wa Kiswahili wanaofundisha shuleni Kiswahili cha kona kama kile kilichoshamiri katika nafasi za umma, basi changamoto zetu ni nyingi na nzito kuliko tulivyokuwa twafikiria awali. Hali yetu mahututi.

Kile ambacho mpaka leo sikielewi ni kwa nini Kiswahili kizuri, Kiswahili sanifu hakipati mwanya wa matumizi katika nafasi za umma. Nauliza kama nilivyowahi kuuliza awali, Kiswahili sanifu kina makosa gani hadi ikawa ni haramu kutumika mwahala mote? Je, siku hizi inakuwa makosa kutumia Kiswahili sanifu kisichokuwa na makosa? Mbona si makosa kuzungumzia au kuandika Kiingereza kisichokuwa na makosa?

Lakini ukitazama tangazo la lile biashara linalonadi nafasi za ajira ughaibuni unaelewa kiini cha matatizo yetu: kutojipenda. Waliounda neno “majuu” kumaanisha nchi za nje, walifanya ubunifu mkubwa unaobainisha si tu kutojipenda bali pia kujichukia. Nchi za watu zimeitwa “majuu” kuashiria ubora wa huko na kwa hiyo uduni wa kwetu huku.

Dhana ya kwamba kule nje maisha ni bora zaidi ya mnyanyaso tunaopitia huku kwetu imekita mizizi. Waafrika wengi wapo radhi kufilia mbali wakijaribu kuvuka jangwa la Sahara au kuvuka bahari ya Mediterranean kwenda “majuu” ambako kiwango cha maisha kipo juu. Nilipoandika hadithi yangu ya ‘Ndoto ya Amerika’, nilikusudia kushadidia na kukejeli uzuzu huu wa kupapia vya wenzetu na kutamanitamani kwa wenzetu.

Sasa hivi ni rahisi kuhitimisha kwamba hawakusibu wahenga waliposema, “Chako ni chako, kikioza kikaushe” au waliposema “Mwache kiwi na chema kimpotele.” Kama wanavyowania kuguria kwengine Waafrika wengi, ndivyo vilevile wanavyong’ania kuzichukia nchi zao na usuli wao.

Isitoshe, sio tu kwamba wanaondokea kupenda lugha za wageni, bali pia wanaziona bora kuliko zao asilia. Hauwapigi mshipa wanapoyachanganya kiholela maneno ya Kiswahili na yale ya Kiingereza. Maneno ya Kiswahili kama kazi au ajira yanakuwa kwao hayana uhondo, yenye uhondo ni ya Kiingereza kama kama job, maneno yanayotoka majuu.

Sijui kama kuna watu wanaojichukia kama sisi duniani. Hakuna chetu tukionacho kizuri. Labda tulikufa kitambo daima tumekuwa maiti kwenenda. Ndiyo, maana hata tukienda majuu kama waendavyo baadhi yetu Arabuni na kudhulumiwa, hatujali sana maana ni kama sisi wenyewe maiti. Tunaelekea kujitia kitanzi kilugha hatujitambui.