Makala

KINA CHA FIKIRA: Ni busara kufikiri kabla ya kusema, maneno hayarudi kinywani yakishatoka

September 23rd, 2020 2 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

KUSEMA ni kuwasiliana na kuelewana.

Mtu husema kitu anachokitaka ndipo hupewa au hununua ama hujitengenezea.

Kusema ni kuzuri mtu akisema vizuri! Lakini ni hatari zaidi mtu anaposema bila kufikiria anachotaka kusema! Anataka kusema na nani? Anataka kusema akiwa wapi ili upate nini? Ni muhimu kufikiri kabla ya kusema badala ya kusema kabla ya kufikiri kwa sababu maneno yakishatoka mdomoni, hayatarudi tena!

Bwana Ulimimoto alikuwa na shamba kubwa la mahindi kijijini Kukumbuzi. Jirani yake, Bwana Theluji alikuwa mfugaji wa ng’ombe na mbuzi. Wote waliishi vizuri kwa amani, upendo na umoja kama ndugu kijijini Kukumbuzi. Walisaidiana kila wakati kwa hali na mali. Tuwapongeze sana kwa hayo!

Siku moja ng’ombe wa Bwana Theluji aliingia kwenye shamba la Ulimimoto kula mahindi.

Theluji alikimbia haraka kumtoa ng’ombe huyo shambani kabla hajala sana mahindi! Ulimimoto alipotokeza na kumwona Theluji akimtoa ng’ombe shambani, alipiga kelele kwa hasira! Akamtukana Theluji vibaya sana! Alimalizia kwa kusema, “Unaringia ng’ombe na mbuzi waliokonda kama wewe! Pia hawana thamani kama mahindi yangu! Ukikanyaga tena shamba langu na huyo ng’ombe wako, nitakuua!” Theluji hakusema chochote!

Wanakijiji wa Kukumbuzi walisikitika na kushangaa sana kusikia Ulimimoto alivyomtukana Theluji! Wengine waliudhika wakasema Ulimimoto apelekwe kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili akachunguzwe ubongo! Lakini wengine walikataa wakasema, “Ugonjwa wa wazimu hakuna! Ni tabia na mazoea tu ya watu kujifanya wamerukwa na akili ili waropoke maneno bila kufikiri! Ulimimoto ashtakiwe tu ndipo ashike adabu!”

Lakini hatimaye Ulimimoto alikubali kuomba msamaha. Wanakijiji waliandamana kumpeleka kwa Chifu Fikirini akaombe msamaha. Walipofika, Ulimimoto alipiga magoti chini akasema, “Naomba msamaha kwa maneno ya ovyo na matusi niliyoyaropoka kumtukana Bwana Theluji! Ninajuta sana! Nyote mnisamehe! Sitarudia tena!”

Chifu Fikirini aliwatazama wanakijiji akasema, “Ni vibaya sana kuyatamka maneno ovyo bila kufikiri kwanza!”

Akanyanyuka na kuingia ndani ya nyumba. Kisha alitoka na kikapu kilichojaa manyoya ya kuku. Alimpa Ulimimoto akimwambia, “Chota manyoya hayo uyarushe hewani mpaka yaishe kikapuni!”

Kila mtu alitazama jinsi Ulimimoto alivyoyarusha manyoya hewani mpaka yakaisha!

Bwana Chifu aliwauliza wanakijiji, “Nyote mmeona?” Wakajibu, “Ndiyooo!” Chifu alimgeukia Ulimimoto akamwambia, “Sasa uyakusanye manyoya yote uliyoyarusha hewani uyarudishe kikapuni!”

Looh! Manyoya yote yalipeperushwa na upepo yakaenda kila upande hewani! Hayakusanyiki tena yarudishwe kikapuni! Ulimimoto aliduwaa! Chifu akamwambia, “Hivyo ndivyo maneno yalivyo! Yakishatoka mdomoni hayatarudi tena! Ukiwa hutaki yatoke ili yasisambae, usiyatoe mdomoni! Usiropoke! Ukishayatoa, hata ukiomba msamaha, hayatarudi!”

Ndugu wapenzi, fikiri kabla ya kusema! Usiseme kabla ya kufikiri! Maneno ni kama manyoya, yakishatoka, hayarudi tena!!