Makala

KINA CHA FIKIRA: Raha iliyoje Kiswahili kufundishwa rasmi katika shule za msingi Uganda

December 4th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

NIMESOMA habari njema kuhusu maendeleo ya Kiswahili Uganda.

Habari njema kwa sababu maendeleo ya Kiswahili Uganda yamekuwa ya kusuasua.

Kuanzia mwaka 2020 Kiswahili kitaanza kufundishwa kama somo la lazima katika shule za msingi Uganda.

Hilo kwangu ni la kufurahisha na kufariji sana.

Nimewahi kuelezea kwenye safu hii ya Kina cha Fikra na kwenye kumbi mbalimbali za magazetini na nje ya magazeti kwamba mkakati wa ufundishaji wa Kiswahili Uganda ni mbaya.

Si mbaya tu bali mkakati kombo hasa kwa sababu Kiswahili kilikuwa tangu hapo kinafundishwa kutokea tu shule za upili kama somo la hiari. Yaani ni labda Uganda tu ndiko ambako watu walikuwa wameamua kukwea mtu kutokea juu.

Inanikumbusha hekima ya rafiki yangu wa zamani Geoffrey Lukalo kwamba ni katika kuchimba kisima tu ndicho watu huanzia juu wakienda chini. Nasema labda, kwa sababu yamkini Rwanda nao wanalo tatizo lilo hilo la kuanza juu na kwenda chini: Kiswahili kinafundishwa tu kutokea shule za upili.

Kwa hiyo taarifa kwamba Uganda wameamua kuanzia ufundishaji wa Kiswahili katika shule za msingi tena kama somo la lazima, zimefurahisha si haba.

Rafiki zangu Wanauganda (ninajiepusha hapa kusema Waganda maana hilo ni kabila moja tu miongoni mwa makabila mengi) wameniambia Uganda sio tena pahala pa kukipigania Kiswahili.

Kwao wao Kiswahili kimeshashinda vita na wapiganaji kama Prof Ruth Mukama na Prof Austin Bukenya na waliokuja baada yao ili kupua fataki, mizinga na mabomu ya kitamathali katika kukikweza Kiswahili hawana budi kubwaga silaha sasa. Yaani kwao wao mambo yamekitengenekea Kiswahili nchini Uganda.

Ni kweli kwamba mfumo wa ufundishaji wa Kiswahili katika shule za upili Uganda umekuwapo. Walimu wa Kiswahili wa shule za msingi wamepewa mafunzo na hawana shule za kufundisha.

Kwa hiyo, habari kwamba kitafundishwa rasmi kwenye shule za msingi zinatoa matumaini kwa walimu hawa wahitimu waliokuwa kama pakacha bila mazao. Hizo ni habari njema Kabisa.

Isitoshe, kwa mara ya kwanza Uganda itakuwa mwenyeji wa kongamano la Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (Chaukidu) kuanzia Disemba tarehe 14, mwaka huu wa 2019. Kuandaliwa kwa kongomano la chama hiki kilichoasisiwa katika mji wa Madison, jimbo la Wisconsin, Marekani na kuvutia uanachama katika pembe zote za dunia, ni tukio kubwa.

Tayari makongomano kadha ya Chaukidu yameandaliwa Nairobi na Zanzibar.

Kwa ambavyo Uganda imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya Kiswahili, kwa kweli inastahiki na kustahili kuwa mwenyeji wa kongomano la hadhi kubwa kama hili la Chaukidu. Hongereni waandalizi wa kongomano mkiongozwa na Aidah Mutenyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kyambogo.

Hata hivyo, nashauri Uganda wasifikirie kwamba mapambano ya ajili ya kukiendeleza Kiswahili yamekwisha. La hasha. Huu ni mwanzo tu. Mathalan wapo wazalendo wa Kiganda wanaodhani kwamba Kiswahili kinatishia mustakabali wa Kiganda chao. Mapambano bado yanaendelea.