Makala

KINA CHA FIKIRA: Sawa na Kiingereza, kuna Kiswahili na 'Viswahili' ainati

October 9th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

NI rahisi sana kudhani kwamba ipo lugha moja hivi iitwayo Kiingereza duniani.

Ni hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyesema kwamba “Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia.”

Na hilo ni kweli kitamathali, nami katika hafla nyingi ninakoalikwa na nikakwenda kwa kudoea, huwa ninamnukuu Mwalimu Nyerere.

Labda nisisitize kwamba bado kuna waungwana wanaoridhia kunialika katika hafla zao nami nashukuru sana kwa ufikirio wao.

Kwa hiyo tunaweza kuchukulia kwa jumla kwamba ipo lugha iitwayo Kiingereza. Lakini ukichungua kwa makini kwa kweli utaona hakuna lugha ya Kiingereza.

Kiingereza kipo wapi? Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba vilivyopo ni Viingereza; tena vingi sana vilivyotandawizwa katika tufe zima la dunia.

Kila uendapo unakutana na Kiingereza cha huko, Kiingereza cha Marekani Magharibi, Kiingereza cha Marekani Kusini (Si Amerika ya Kusini), Kiingereza cha Katikati mwa Marekani, Kiingereza cha India, Kiingereza cha Uganda, Kiingereza cha Kenya, Kiingereza cha England, Kiingereza cha Ireland Kaskazini.

Ilmuradi unachokumbana nacho katika jumla la mambo ni mchafukoge wa ‘Viingereza’ vinavyohitalifiana ingawa mawasiliano bado yanawezekana kuwapo kati ya wasemaji wa janibu hizi mbalimbali.

Hivi Viingereza vinaitwa “Englishes.” Na Kiswahili je? Je, hivi kuna lugha inayojulikana kama Kiswahili? Ndiyo. Lakini pia sharti tukiri kwamba kwa mantiki tuliyoitumia kufikia hitimisho kwamba vipo Viingereza vingi, basi hali kadhalika kuna Viswahili vingi vilivyotapakaa katika janibu mbalimbali. Kamwe hatupaswi kujificha katika kwapa za kile Kiitwacho Kiswahili sanifu na kuupuza kweli hii ya kuwepo kwa Viswahili vingi.

Hivi karibuni nilikuwa ninahariri makala ya kitaaluma iliyoandikwa na msomi mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Alinifumbua macho kuhusu kasumba tuliyo nayo kwamba sharti tuseme sote Kiswahili kimoja.

Hilo haliwezekani. Kwa kweli alichokisema msomi yule wa Kongo ni kwamba watu wa kwao wamekerwa na kuchekwachekwa na wenzao wa Afrika Mashariki kwa kusema Kiswahili tofauti. Wanakerwa sana. Yaani kila wakifumbua vinywa kuzungumza, wenzetu hasa wa Tanzania na Kenya, huwa wanapasuka kwa vicheko vya kejeli na dharau. Watu wa Afrika Mashariki hawakuzoea Kiswahili cha “gavementi,” (serikali) “mnyumba,” (nyumbani) “tuko mu distraction,” (tunakengeushwa) “Yeye yuko nafasi nzuri kufahamu,” (yeye anaweza kufahamu vizuri) “acha nikupe hii numero akuite” (acha nikupe nambari hii ili umpigie simu).

Hata mimi sikielewi sana Kiswahili hiki cha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ndio maana nadhani huenda juhudi zangu za kutafsiri baadhi za kauli hapa zikawa hazijafua dafu vilivyo. Wakisoma wenyewe wanaweza kubaini makosa yangu ya tafsiri. Au yamkini wewe msomaji wangu mwenyewe wayaona makosa yangu ya kitarjumi. Lakini alichosema msomi huyo wa Kongo ni kwamba, “Jamani acheni kutucheka.” Tusiwacheke wenzetu.

Kwa hiyo tufikia hitimisho gani? Kwamba kwa jumla tunaweza kusema kuna Kiswahili duniani na pia hakuna Kiswahili; kuna Viswahili. Tuache kuchekana. Tuache kukisongoa Kiswahili. Tuseme Kiswahili kisichokuwa na kona.

Tunajenga nyumba moja tusipiganie fito.