Makala

KINA CHA FIKIRA: Shirikiana na watu bora ili nawe uwe bora, visivyo utasalia bure tu!

November 11th, 2020 2 min read

NA WALLAH BIN WALLAH

KATIKA maisha ubora hutafutwa kwa hali na mali. Lazima ukae na watu walio bora mahali palipo na ubora ndipo ujifunze ubora ili uwe bora! Ubora ni ghali wala haupatikani bure bure bila ya kujituma na kujitahidi mpaka uzipate mbinu zitakazokusaidia kuwa bora!

Kwa mfano, ukitaka kujifunza elimu au maarifa fulani, unapaswa kukaa na wenye elimu hiyo na maarifa unayoyataka ili ujifunze au wakufunze uwe mtaalam mwenye ubora kama wao.

Huwezi kuwa mchezaji bora wa kandanda bila ya kushirikiana na wachezaji walio bora kufanya mazoezi pamoja uwanjani. Ni vigumu kuwa mkulima hodari bila ya kuenda shambani pamoja na wakulima wanaojua hali ya anga na mimea mbalimbali.Ukitaka kuwa mvuvi lazima ujue mazingira ya majini pamoja na tabia za samaki wote ukielekezwa na wavuvi wakongwe.

Kujifunza ndiko kuelewa mambo. Nako kujifunza ni kutafuta ubora kama unavyojifunza ujenzi, hisabati, sayansi, ufasaha wa lugha, uandishi wa habari na mengineyo kutoka kwa wataalam wenye ubora wakusaidie kuwa bora!

Vivyo hivyo, ukitaka kuupoteza ubora wako, enda ushirikiane na watu ambao hawana ubora wowote! Baada ya muda, utakuwa kama hao hao! Ujifunze kila wakati ili ujiboreshe kila siku.

Kinolewacho hupata! Na kikipata hukata!Bwana Tuishi alienda kutembea msituni. Akaona kiota cha ndege aitwaye tai. Kiota hicho kilikuwa na mayai! Tai ni ndege mwenye macho makali yanayoona mbali sana.

Tai ana nguvu nyingi, kidona kikali na kucha zenye ncha kali za kumrarua mnyama yeyote akaliwa nyama! Aidha tai ana mbio zaidi za kupaa angani kuenda masafa marefu!Bwana Tuishi alilichukua yai moja katika kiota cha tai akapeleka nyumbani na kuliweka pamoja na mayai ya kuku wake aliyekuwa akiyaatamia mayai kwenye oto!

Baada ya siku kadhaa, kuku wa Bwana Tuishi aliyaangua mayai yote pamoja na lile la tai! Vitoto vyote vya kuku na cha tai vilikua pamoja na kutembea pamoja vikidonoa punje za nafaka na vijitakataka vingine ardhini!Kwa hakika, Bwana Tuishi alitarajia kuona kwamba kitoto cha tai kingeruka angani siku moja kama tai wengine aende zake, lakini wapi!!

Kilitembea kufuatana na vifaranga mpaka vifaranga vilipokuwa kuku wakubwa! Naye tai akawa mkubwa lakini hakuruka kabisa angani! Aliupoteza ubora wake wa kawaida ya tai kupaa angani kwa sababu aliishi na kuku wasiopaa angani!Ndugu wapenzi, usipojitambua mapema, utaupoteza ubora wako wakati wa kushirikiana na watu ambao hawana ubora unaoutamani wewe na unaopaswa kuwa nao maishani!!!

[email protected]