Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KINA CHA FIKIRA: Taaluma ya Kiswahili yahitaji asasi madhubuti kuboresha utumizi wake

January 8th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

PROF Kimani Njogu amewasha kiberiti cha moto ambao ulitishia kuteketeza msitu mkubwa alipouliza hivi karibuni kwa nini istilahi “literary stylistics” imetafsiriwa elimumtindo na baadhi ya wanataaluma.

Unapojaribisha kitu ili kuona matokeo yake yatakuwaje au yatakuwa nini, tunaweza kusema “unatingisha kiberiti ili kuona kama ndani mna njiti” katika Kiswahili cha kisanii.

Prof Njogu hakuwa anatingisha tu njiti, ameuliza swali la kuchochea mjadala mpevu kuhusu usahihi wa baadhi ya istilahi zinazotumika katika taaluma za Kiswahili. Kama hatuwezi kuanza kusaili baadhi ya istilahi na mikondo na mikabala tutakuwa tunazihini taaluma fursa ya kwenda mbele.

Kiswahili mbele hakiendi pasi na kuuliza maswali yenye mwelekeo wa kimapinduzi, maswali yanayokaribiana na kufuru. Hatuwezi kuendelea kuafikiana na maneno na istilahi zilizoko na hata kanuni za sarufi kimsobemsobe tu. Sharti tusitawishi tabia ya kusaili na kujisaili. Prof Kimani kauliza kuna uhusiano gani kati ya istilahi ya Kiswahili elimumtindo na literary stylistics?

Nao wachangiaji wakachochewa kutoa maoni mbalimbali yanayokinzana. Kama utanzu wa taaluma, stylistics inajishughulisha na matumizi ya mitindo katika kazi za fasihi. Kwa hiyo naungana na Prof Kimani na wengine wanaosema kwamba istilahi elimumtindo labda ni tafsiri kombo kwa vile inajikita hasa katika tasnia ya elimu. Nasema labda kwa vile, kwa baadhi ya wasomi, nadhani Prof Hermas Mwansoko na Prof Kineene wa Mutiso wamo humu, neno la Kiingereza “study” linaweza kutafsiriwa kama elimu kwa Kiswahili na wala sio elimu kama kisawe cha neno la Kiingereza “education” tu.

Ndiyo maana mnajimu anaweza kuelezewa kama mtaalamu wa elimu ya nyota, kabobea na kutopea (huu uradidi ni mtindo wa Wallah bin Wallah) kwenye taaluma au elimu (study) ya nyota.

Je, mijadala kama hii itaishia kwenye kumbi la jamii mitandaoni au itaifikia asasi mahsusi zinazohusika na kutoa miongozo na maelekezo thabiti ya matumizi ya lugha katika taaluma za Kiswahili? Hapa ndipo kwa kweli tunapohitaji Baraza la Kiswahili la Taifa linalotenda, lenye meno yanayong’ata (tafsiri mbaya hii, sio?). Upo mwamko mwema wa kusailisaili. Mwamko huu si tu katika swali la Prof Kimani Njogu bali katika mambo mengine mengi. Kila mwamko huu ukijitokeza katika taaluma hizi za Kiswahili, ipo haja kujenga utamaduni wa kushirikiana na kushauriana, si kushindana na kuhamisiana na kufikia mahitimisho yanayojenga taaluma.

Ninahisi taaluma za Kiswahili zimejaa kelele nyingi mno zinazopigwa kiholela na wamba-ngoma kadha wa kadha, kila mmoja akivutia kwake. Hizi kelele ni nzuri ila zinaonesha kwamba ipo haja kuwa na vyombo vya kuzidhibiti.

Kelele hizi hazipaswi kuanzia na kuishia kwenye kumbi la kijamii mitandaoni. Waama, kelele hizo zinaonesha hamkani si shwari tena na kama asasi zilizopo hazikidhi haja, wakereketwa watajiundia wenyewe asasi mbadala za kimapindukizi na kuchapusha ukuzi wa Kiswahili.