Makala

KINA CHA FIKIRA: Twaweza kukimakinikia Kiswahili na kukisarifu ipasavyo madhali nia ipo

November 20th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

BAADHI ya wasemaji wa Kiswahili hawana habari kuhusu tofauti iliyopo kati ya tunda la limao na ndimu. Ukienda sokoni kununua ndimu aghalabu utapewa limau.

Ajabu ni kwamba tatizo hilo halipo tu kwa wanunuzi bali hata kwa wauzaji wa matunda haya sokoni. Unaweza kukumbana na tatizo hilo, si hoja upo soko la Kongowea, Mombasa au Soko Mjinga kwenye eneo la Fly Over. Vile ninavyoelewa mimi katika Kiswahili changu duni, tunda linaloitwa kwa Kiingereza “lemon” ndilo kwa Kiswahili tunaliita limau.

Kwa upande mwingine tunda lile linaloitwa “lime” katika Kiingereza ndilo katika Kiswahili tunaliita ndimu.

Mchanyanyiko huu wa mambo kilugha imekita mizizi sana katika matumizi ya Kiswahili.

Miaka michache iliyopita niliwahi kuzungumzia katika safu hii tatizo la kubaini aina za pilipili, yaani kupambanua baina ya pilipili hoho na pilipili mboga. Si wanunuzi si wauzaji, utawasikia wanazichanganya sana aina mbili hizi za pilipili. Sio wengi wanang’amua kwamba pilipili hoho ndiyo ile kali kabisa na kwamba jina lake “hoho” linabeba maana ya mwasho wa ukali wa pilipili aina hii.

Si ajabu basi kuwasikia watu wakisema watoto vijana na wasichana, badala ya wavulana na wasichana. Haiwapitikii akilini kwamba wasichana pia ni vijana kama wavulana. Wanachanganya baina ya neno kijana na mvulana, na kusahau kwamba neno kijana ni jumlishi zaidi wala halibagui watoto wa kike.

Aidha utawasikia watu wakisema “karaya” badala ya “karai” wanaporejelea chombo cha kutekea maji na kuogea au kunawia. Na kwa sababu nimelitaja neno “nawa,” hilo nalo lina utata. Baadhi ya wasemaji utawasikia wakisema mambo kama vile, “oga mikono au uso” badala ya “nawa mikono au uso.” Kwa ninavyoelewa mimi haiwezekani kunawa mikono na nyuso. Tunaosha au kunawa tu basi.

Makosa aina hii huwa yanatarajiwa siku hizi ninapotagusana na wananchi wenzangu, walalahoi kama mimi.

Kwa hiyo nilishangaa niliposafiri hivi karibuni hadi kwenye soko la Ekero kwenye barabara kati ya Mumias na Kakamega. Niliingia kwenye mgahawa mmoja miongoni mwa migahawa mingi inayowahudumia wapitanjia na wenyeji wa Ekero.

Nilishangaa sana mhudumu au hadimu alipouliza: “Nani atakula ugali kwa kuku?” Nilishangaa kwa vile nilitarajia avunje kanuni za sarufi kama ilivyo ada ya wasemaji wengi wa Kiswahili. Nilipomwuliza jina lake aliniambia anaitwa Hamisi. Hivyo, Hamisi na wenzake wa Ekero waling’amuaje usahihi wa sarufi? Mbona Kiswahili kinawatoka vizuri kwa mazoea?

Kusema la haki nilimsifu na kumpongeza sana Hamisi kwa umilisi wake mwafaka wa lugha arifu ya Kiswahili.

Hamisi ni ithibati nyingine kwamba mtu akitaka kusema Kiswahili safi, atakisema bila tashwishi. Penye nia pana njia na penye msemaji mzuri wa lugha kuna uzuri na uhondo.

Ninachouliza ni je, kwa nini Wakenya wasijitolee sabili kama hadimu Hamisi kukisema Kiswahili ipasavyo? Kwa nini Kiswahili kutwa kucha kinaendelea kutumiwa kama kopo la msalani?