Makala

KINA CHA FIKIRA: UG kuwa mwenyeji wa kongamano la CHAUKIDU Disemba

October 16th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

MNAMO Jumatatu wiki hii nilimwambia Rais wa Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani, (CHAUKIDU), Profesa Leonard Muaka kuhusiana na kongomano la chama hicho linalotarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Kyambogo, Uganda Disemba 2019.

Naomba bora nidondoe barua nzima kama nilivyomwandikia hapa chini:

Mpendwa Ndugu Rais,

Kwa heshima na taadhima tunakuleteani ikisiri ya jopo letu la waandishi kama tulivyokuahidini. Wanajopo wote wameridhia kushiriki. Nasi twashukuru kwa CHAUKIDU kuridhia kutowatoza ada za kiingilio wanajopo wa jopo hili maalum. Ilieweke kwamba kwengineko waandishi wa fasihi bunilizi wanapoalikwa kwenye makongomano huwa wanaowalika wanagharimia na wala si kinyume chake. Lakini haidhuru tunaelewa hali ya chama kwa sasa. Baadaye tutalifikiria hilo kwa uzito. 

Mwisho, twaomba barua za ukubalifu wa ikisiri na mialiko rasmi ili baadhi ya  wanajopo wawasiliane na wakuu wao kazini  kuanzisha mchakato wa kupata ufadhili.

Shukran sana mheshimiwa Rais.

Nduguyo Ken Walibora

 

Nimemwandikia Rais wa CHAUKIDU, chama ambacho nilikuwa ndiye rais wake wa kwanza kilipoasisiwa kule Marekani mjini Madison, mnamo Aprili 2012.

Mheshimiwa Rais wa chama ameniomba niunde jopo la waandishi wa bunilizi za Kiswahili ambao watashiriki katika kongomano hili la kistoria litakalofanyika kwa mara ya kwanza katika kile kiitwacho ‘lulu ya Afrika’ yaani nchi ya Uganda.

Tayari Kenya imeshawahi kuwa mwenyeji wa kongomano la Chaukidu mnamo mwaka 2016 kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Catholic, mtaani Karen. Tanzania nayo ikawa mwenyeji mnamo 2018 huko Zanzibar.

Mikutano mingine yote ya Chaukidu imekuwa hususan Marekani, ukiwemo mkutano uliofunguliwa rasmi na rais wa awamu ya pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Ilikuwa heshima yangu kuhusika katika usawidi na uhariri wa hotuba (au kama anavyosema mtangazaji mkongwe Charles Hillary, hutuba) aliyoitoa rais mstaafu.

Rais wa chama aliponiomba, niliitika wito wake mara moja nao waandishi wenzangu niliowasiliana nao waliridhia mara moja kama ninavyosema katika barua yangu hapo juu.

Lililopo ni kwamba kama kamati andalizi italeta majibu chanya kwa uwasilisho wa ikisiri yetu tutapata fursa ya kujadili na wajumbe wa kongomano kuhusu vipengee muhimu wa kubuniliza (neno la Prof Mwenda Mbatia).

Tunadhamiria kushirikisha wajumbe tajiriba yetu ya uandishi kuhusu mathalan, wapi inapotokea kariha yetu? (au tunaandika bila kariha ni sulubu tupu?),  nini dhamira ya uandishi wetu? Wapi yanapotoka maudhui ya kazi zetu? wahusika wanaibukaje na tunawaumbaje? Msuko wa hadithi tunausukaje? na hadithi inatokezea wapi? Vitushi tunavyopingaje? Itikadi ina dhima ipi katika kubuniliza? Twasemeje kuhusu urithishaji wa mikoba ya uandishi tukiwa tunachungulia kaburi au karibu twende njia ya marahaba? Tunatoa nasaha gani kwa waandishi chipukizi na watarajiwa? n.k.

Mimi nina hamu kubwa ya kushiriki kwenye jopo hili. Natumai nitapata ufadhili wa kwenda Kyambogo. Nikikosa nitatembea pekupeku nikafike. Ila nachosema tukiwathamini waandishi, hatutaona tabu kuwadhamini kila tunapowahitajia. Au tusubiri wavunje rekodi kama Eliud Kipchoge?