Makala

KINA CHA FIKIRA: Uhasama na mihemko ya kitaifa na kizalendo inavyotishia mustakabali wa lugha ya Kiswahili

October 23rd, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

NOAH Webster alibaini kwamba si tu Kiingereza cha Marekani kilikuwa tofauti na cha Uingereza kwa msamiati, tahajia na matamshi, bali pia kulikuwa tofauti kubwa katika Kiingereza cha Wamarekani wenyewe kwa wenyewe.

Kwa hiyo alidhamiria kukisanifisha Kiingereza cha Marekani ili kujenga uelewano zaidi na pia kujenga tahajia mpya inayowaafiki wao.

Katika kuunda kamusi ya Kiingereza cha Marekani, Webster alitomea vidahizo takriban 70,000 ambapo vidahizo 12,000 havikuwa vimewahi kupachikwa kwenye kamusi yoyote.

Ili kutimiza azma yake, ilibidi ajifunze jumla ya lugha 26, nami hilo silioni kama dogo!

Kwa hiyo, Webster alifanikiwa ‘kuikomboa’ Marekani, ambayo ilikuwa koloni ya Waingereza kutoka kwa minyororo ya kanuni na kaida za Kiingereza cha Uingereza.

Webster alifanikiwa kuikomboa kamusi ya Kiingereza cha Marekani kutoka kwenye mikatale ya kamusi ya Oxford Dictionary yenye mamlaka tangu hapo kote duniani penye msambao wa Kiingereza.

Aliona kwamba tahajia za Uingereza zilikuwa za kutatanisha, kwa hiyo akajasiria kudondoa herufi ‘u’ katika baadhi ya maneno kama vile colour (likawa color), vapour na (likawa vapor), na akabadili waggon kuwa wagon, na centre kuwa center.

Toleo lake la kwanza mnamo 1806 lilimfilisisha; aliuza nakala kama 2500 tu. Alipotoa toleo la pili ndipo alianza kupata tija kiasi.

Kitu kama hicho kinatokea Uswahilini? Kuna sintofahamu inayotokota kati ya Kiswahili cha TATAKI na BAKITA cha Dar es Salaam na Kiswahili cha Bakiza cha Zanzibar.

Unaweza kufikiri hali ni shwari, kwamba Wazanzibari wanasema Kiswahili chao na kuridhika nacho na wasemaji wa Tanzania bara watasema Kiswahili chao na kukinai. Lakini kweli ni kwamba kuna uhasama na mihemko ya kitaifa na kizalendo inayotishia mustakabali wa Kiswahili.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu ilipotungwa na kuchapishwa 1981 ilidhaniwa kuwa ilijikita katika msingi wa Kiswahili sanifu cha Unguja, lahaja iliyoteuliwa na Wakoloni kuwa lugha ya mawasiliano mapana kote kunakozungumzwa Kiswahili.

Lakini labda fikra za kitaifa za visiwani zinasaili kwa nini Kamusi ya Kiswahili Sanifu, kinachosemekana kilitoka Zanzibar, ichapishwe Dar es Salaam. Jibu kwamba ni Dar es ndiko ilikokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (sasa TATAKI) halizimi wimbi la fukuto la kitaifa la Wazanzibari.

Kwa hiyo kuchapishwa kwa Kamusi la Kiswahili Sanifu, ni uasi dhidi ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Isitoshe, Wanzibari walienda hatua zaidi na kutunga ‘makamusi’ ya Kimakunduchi, Kipemba, na Kitumbatu. Je, wanajaribu kujikomboa kutoka kwa ukoloni wa kiisimu na kitaaluma wa Tanzania bara? Je, Kiswahili sanifu si lugha mpya kwa kweli? Au ni lugha ya Dar es Slaam ama Zanzibar?

Nilishuhudia hivi karibuni cheche za kuchambana kati ya baadhi ya wasomi wa Tanzania bara na wale wa visiwani na wakereketwa wao katika mitandao ya kijamii. Vuta n’kuvute hii ni dalili ya tatizo kubwa kuliko tunavyotaka kukiri.

Tutajengaje nyumba moja na tunapigania fito?