Makala

KINA CHA FIKIRA: Usijipalie makaa kwa kuyachezea maisha yako mwenyewe

July 1st, 2020 2 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

KITENDO chochote anachokitenda mwanadamu maishani, kikiwa kizuri au kibaya, ni kwa ajili yake yeye mwenyewe!

Kila mkulima huvuna alichokipanda. Bidii za mtu ndiyo mafanikio yake. Na uzembe wa mtu ndiyo majuto yake maishani! Kadhalika, kufaulu na kutofaulu kwa mwanafunzi masomoni hutegemea kazi na bidii zake mwenyewe. Lakini masikitiko ni kwamba wanafunzi wengine hawajui kuwa wanasoma kwa maslahi yao wenyewe wala si kwa faida za walimu na wazazi wao! Ole wao wanafunzi kama hao!

Sakubimbi, mwanafunzi wa shule ya Sirimoyoni. Alikuwa mwenye machachari na kiherehere shuleni Sirimoyoni. Alitaka kila mtu amtambue. Alikuwa mchangamfu darasani lakini mtoro aliyetoroka mara nyingi kutoka shuleni! Kwa jumla Sakubimbi alikuwa mwenye tabia na sifa zisizoridhisha. Alizoea kuenda shuleni akiwa amebeba maandazi, chapati na pesa za kununulia peremende katika kantini ya shule. Kilichomkera kila mtu shuleni hapo ni kwamba Sakubimbi alipenda sana kupigana na wanafunzi wenzake!

Walimu waliamua kuwaita wazazi wa Sakubimbi ili waelezwe kuhusu tabia na mwenendo wa mtoto wao! Wazazi walishtuka na kushangaa sana walipoambiwa kila kitu! Walisema kwa kuapa kwamba, “Sakubimbi mtoto wetu ni mwema, mpole na mwenye heshima sana kwa watu wote nyumbani na majirani!” Walimfananisha na Malaika watumishi wa Mwenyezi Mungu! Wazazi hawakuyaamini maneno ya walimu! Wanafunzi wenzake Sakubimbi waliitwa kutoa ushahidi na maoni yao. Kisha Sakubimbi mwenyewe alikiri kwamba maneno yote yaliyosemwa dhidi yake yalikuwa ukweli kabisa! Hapo ndipo wazazi waliposhawishika kuamini walivyoambiwa!

Kwa hakika, watoto wabaya au watu wabaya huwa wana sura nyingi na tabia nyingi. Kila sura na tabia hizo hutumiwa mahali fulani maalum! Akina Sakubimbi wakiwa mitaani huonyesha sura na tabia za mitaani. Wakiwa shuleni, hutumia tabia na sura tofauti! Wanapokuwa nyumbani hutumia sura na tabia nyingine tofauti kabisa ili kuwaziba macho wazazi, ndugu na jamaa! Lakini zote hizo ni mbio za sakafuni ambazo huishia ukingoni! Wahenga walisema, “Ukiuficha motO, moshi utakufichua!”

Ndugu mlezi au mzazi, unapomlea mwana usiangalie upande mmoja tu wa malezi kwamba, “Mtoto anaenda shuleni na kusoma vizuri!” Chunguza pande zote za tabia na vitendo kwa undani zaidi! Tangu janga la virusi vya korona lilipotangazwa na shule zote kufungwa ili wazazi wakae na watoto wao majumbani, wamejionea sura mpya na tabia mpya ambazo hawakuzijua kwa watoto wao! Hilo ni fundisho kubwa kwetu sisi sote! Lakini muhimu zaidi ni wasia na onyo kwa kila mtoto, mvulana na msichana, “Wewe mwana, uache kabisa kuyachezea Maisha yako! Unapoyachezea Maisha yako, unajichezea wewe mwenyewe!” Zingatia!!