Makala

KINA CHA FIKIRA: Viongozi wa Afrika Mashariki ni wasaliti wa Kiswahili barani

July 17th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

MUUNGANO wa Afrika umepanga mikakati kabambe ya kukipa Kiswahili kipaumbele kama lugha ya mawasiliano mapana barani. (Mimi si miongoni mwa watu wanaoona ni sawa kutafsiri Afrika Union kama Umoja wa Afrika kwa sababu tukifanya hivyo tutatafsiri vipi Organization of African Unity; asasi iliyoitangulia African Union?).

Ni kweli kwamba Kiswahili ni moja katika lugha rasmi za Muungano huo tangu mwaka 2004.

Lugha nyinginezo zote zinazotumiwa katika kutekeleza majukumu rasmi ya Muungano wa Afrika ni Kireno, Kifaransa, Kiarabu na Kiingereza. Kuteuliwa kwa Kiswahili kutumiwa katika vikao vya asasi hii muhimu barani Afrika ulikuwa bila shaka hatua kubwa katika kukienzi Kiswahili.

Hata hivyo, tamko la kukifanya Kiswahili lugha ya matumizi katika Muungano wa Afrika halijazaa matunda yoyote ya kupigiwa mfano.

Viongozi wa Afrika Mashariki hawajathibitisha mapenzi yao kwa Kiswahili kwa kukizungumza kwenye vikao vya Muungano wa Afrika.

Mpaka sasa Kiswahili kinawadai deni kubwa viongozi wa Afrika Mashariki yaani Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda na hata wale wa Afrika ya Kati hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; kwa kukitelekeza Kiswahili licha ya hadhi kubwa ambacho kimepewa katika mawanda rasmi ya Muungano wa Afrika. Kwa hili viongozi wa Afrika si tu kwamba wamefeli vibaya vibaya ila pia wamekisaliti Kiswahili.

Inakuwaje kwamba wanaokitetea Kiswahili wanaondokea kuwa watu wa asili ya kwingineko nje ya Afrika Mashariki?

Inakuwaje kwamba Kiswahili kinapata utetezi wa dhati kutoka kwa watu wasioweza kukisema kama vile kiongozi wa chama cha Freedom Party cha Afrika Kusini, Julius Malema, au mshindi wa tuzo ya nobel ya fasihi Wole Soyinka?

‘Bila Kiingereza hapati huduma’

Inakuwaje kwamba wakati Afrika Kusini inakakania kuanzisha kukifundisha Kiswahili katika shule za msingi, Tanzania inatoa ilani kwa watoto wake “No English no service!”

Nilikuwa jijini Dar es Salaam mwishomwisho wa mwezi wa Juni kuhudhuria kikao cha Akademia ya Lugha za Kiafrika au kwa Kimombo African Academy of Language (ACALAN).

Nilifurahishwa na azma ya asasi hiyo ya Muungano wa Afrika kukifanya Kiswahili moja ya lugha za mawasiliano mapana barani Afrika.

Katibu mtendaji wa ACALAN Dkt Dampha na katibu mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki walionesha nia nzuri ya kushirikiana ili kukiendeleza Kiswahili kote barani.

Ilikuwa fahari yangu kuhusika katika kusawidi Azimio la Dar es Salaam la Uendelezaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika.

Ni dhahiri shahiri kwamba utekelezaji wa azimio la Dar es Salaam utategemea utashi wa kisiasa unaopaswa kuanzia nyumbani kwa Kiswahili ambako ni Afrika Mashariki.

Kwa utashi wa kisiasa namaanisha kujitolea kwa dhati kwa viongozi wa kisiasa wa Afrika Mashariki kuhakikisha kwamba Kiswahili kinapata mashiko thabiti kwanza huku kwetu.

Aidha, viongozi hawa wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kukipigia upatu Kiswahili kwa kukizungumza katika vikao ndani na nje ya Afrika Mashariki.