Makala

KINA CHA FIKIRA: Wakenya wamezoea kuhalalisha makosa ya lugha katika usemaji wao wa Kiswahili

August 14th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

KWENYE Kaunti ya Trans-Nzoia (zamani wilaya) nilikolelewa nilikuwa nasikia maneno fulani niliyodhani ni ya Kiswahili safi.

Mtoto wa ng’ombe au punda aliitwa “njau.”

Chombo cha kutilia maji ili kuoga au kunawa kiliitwa “karaya.”

Mkikutana na mtu mnasalimiana “sana sana,” yaani unamwambia “sana sana,” naye anajibu vivyo hivyo “sana sana.”

Ilinichukua miaka mingi ya ufundishwaji na utafiti kufikia hitimisho kwamba hicho kilikuwa si Kiswahili safi.

Nilikuja kung’amua kwamba maneno sahihi yalipaswa kuwa “ndama,” (badala ya njau) na “karai,” (badala ya karaya).

Aidha nilikuja kugundua kwamba “sana sana” ni mfumo wa mkopo kutoka kwa lugha ya Kibukusu wa salamu “swaswa muno muno,” ambapo uradidi wa neno “muno” lenye maana ya “sana” umeigwa.

Tatizo la watu wa Trans-Nzoia, ni tatizo la Kenya nzima. Ni tatizo la kufanya kosa liwe ndilo jambo la kawaida, jambo lililozoelewa, na lililo sahihi kuonekana kosa.

Bado sina hakika mathalani kama ukisema karai utaeleweka vizuri na baadhi ya watu waliozoea karaya. Mtindo huu wa kuhalalisha makosa ndio uliokita mizizi katika matumizi ya Kiswahili Kenya.

Watu wameuzoea mtindo huu.

Fikiria jinsi kitenzi “zoea” lilivyopata maana nyingine.

Kamusi Kuu ya Kiswahili inasema “zoea” lina maana ya “tabia ya kufanya jambo moja kila mara kwa haraka na kwa kasi.”

Kamusi ya Kiswahili Sanifu nayo inasema “kuwa na hali au tabia ya kufanya jambo moja mara kwa mara kufikia hali ya kutoweza kuepukana nalo.” Vitomeo vya kamusi zote mbili havioneshi kama zoea ni chanya au hasi. Ilmuradi mtu anaweza kuzoea mazuri na mabaya.

Mathalani tunaweza kusema: “Watu wa kaunti ya Trans-Nzoia wanazoea kupanda mahindi kila mwaka.”

Hatusemi kuwa hilo ni jambo zuri au baya. Hatusemi kwamba wanapaswa kuacha kupanda mahindi waingilie kilimo cha maparachichi kwa vile kina tija zaidi.

Aidha tunaweza kusema: “Mashirika ya utetezi wa haki yamezoea kumtetea mtoto msichana pekee.”

Hapa tumeashiria kutelekezwa kwa mtoto wa kiume.

Au twaweza kusema: “Wakenya wamezoea kuhalilisha makosa ya lugha katika usemaji wao wa Kiswahili.”

Katika mifano hii yote tumelitumia neno zoea katika maana yake halisi.

Hata hivyo, maana ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya kulifanya jambo mpaka inakuwa vigumu kuepukana nalo inaashiria kwenye aina fulani ya uraibu.

Mathalani mtu aliyezoea bangi ana uraibu wa bangi.

Nami kwa sasa ninahisi kwamba watu wa Trans-Nzoia na watu wa Kenya kwa jumla wana uraibu wa kuchanganya ndimi wanapozungumza Kiswahili.

Ni uraibu kwa kweli kwa maana hawawezi kujiepusha na huku kuchanganya ndimi. Na wanabirua lugha kabisa. Wakisema “umenizoea,” hawamaanishi zinavyosema kamusi, bali wanamaanisha “hujali tena unanifanyia nini” au “unanidharau.”

Pia wanafikiri wao ni wanafalsafa. Wanakuambia kauli kama “utajua hujui,” na kufikiri wamesema jambo lenye falsafa ya kina. Hamna kitu pale.