Makala

KINA CHA FIKIRA: Wanamuziki wa Kenya wawaige wenzao wa TZ wenye weledi mkubwa wa kukisarifu Kiswahili

August 28th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

WASANII wa Kiswahili wanaoimba muziki wamekuwa wakitia fora sana katika tasnia ya muziki.

Si aghalabu kukutana na raia wa Afrika Mashariki asiyemfahamu walau ahlan wa sahlan wanamuziki kama vile Diamond Platnumz, Akothee na Ali Kiba na Jose Chameleon.

Umaarufu wao umekitwa katika sio tu umahiri wao wa kuimba bali pia katika kusanifu lugha ya Kiswahili.

Siku zote miye nasema wasanii wa Tanzania wanavuma zaidi kwa vile wanajua namna ya kusuka maneno, kusana maneno, kuyasarifu kwa Kiswahili kizuri kitamu, kuyaremba.

Wakenya, isipokuwa wachache kama Akothee wanaroroma roroma tu kwa maneno ya kivoloya.

Wasanii wa muziki Kenya wangesoma vitabu wakajua maneno rahisi matamu ya kuvutia, wangejua namna ya kufinyanga muziki wa kutamananisha.

Sharti mwanamuziki kama vile mwanafasihi wa kusema na kuandika, awe na uwezo wa kubaini ladha ya maneno, ladha ya nahau, na semi na jazanda na tasfida.

Sharti asitawishe vionjo mwenyewe vya utamu na raghba ya kauli, na kina cha falsafa ili muziki wake upendekeze vizazi hadi vizazi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa wimbo wa “Malaika” ambao unaaminiwa ulitungwa na marehemu Fadhili Williams (Mkenya) na kuimbwa naye na wengine wengi ndani na nje ya Afrika Mashariki kama vile Miriam Makeba na Boney M.

Hawa wageni wameuimba wimbo huo wasioujua maana mwanzoni kwa sababu umetungwa ukatungika na kukiuka mipaka ya lugha na jiografia.

Hii leo Wakenya wanarusha rusha tu miparaganyo ya maneno katika muziki wao. Mambo yalianza enzi za Lenny, Mr. Googs and Vinnie Brown na wimbo wenye maneno “wasee tunatoka Githurai tumekam kukupa rhymes zingine dry tukifry.” Kama walitaka kusifia mtaa wa Githurai wangeenda Tanzania wafundishwe utamu wa kutunga na kusifia eneo katika wimbo wa “Kigoma.” Huwezi kuvutia na Githurai ya “wasee tunatoka Githurai,” kama vile unavyovutiwa na uhondo wa “Kigoma aee Kigoma weeeh tunayo furaha… tunayo furaha kuwa wazawa wa Kigoma.”

Ni kama kulinganisha ndovu na panya.

Kunengua

Hata hivyo, hali ya muziki wa Kiswahili Kenya ilianza kuwa mahututi wanamazuki walipogundua kwamba siri ya mafanikio ni kuwaweka wanenguaji waendao tuputupu.

Kisha muziki wa Kenya ulikufa fofofo wakati wanamuziki walipoamua kuchukua njia ya mkato ya kupendwa na wengi kwa kuimba matusi ya moja kwa moja.

Sasa hivi ni vigumu kutafautisha kati ya matusi na muziki nchini Kenya.

Juzi nilipokuwa katika mazishi ya mke wa amu nilimwona mwombolezaji mmoja amekuja na fulana (t-shirt) yenye maandishi ‘Wamnyonyez, Wamlambez!’ Yaani kaja kuomboleza kweli au kaja kulia machozi ya mamba?

Ila hapo ndipo walipotufikisha wanamuziki wetu tunaowaenzi licha ya umaskini wao kwenye ubunifu.

Hapo awali nilikuwa nimekwishaona video kwenye WhatsApp inayoonyesha halaiki mazishini ikinengua huku muziki wa maneno haya ya kutisha ukichezwa.

Hata Watanzania wanaimba matusi, ila ni weledi wa kuteua maneno, hata huwezi kujua mpaka uwe mweledi. Pema hapo?