Makala

KINA CHA FIKIRA: Waswahili wameonyesha utu kumuenzi Maulidi Juma, shujaa wa taarab

February 19th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

WAKEREKETWA kwa Kiswahili wamethibitisha kwa mara nyingine tena kwamba hawana hatinafsi. Hatinafsi ni uroho, ubinafsi, tabia ya kujifikiria mtu mwenyewe tu, roho ya mimi kwanza na mimi mwisho.

Nilisikia mkakati wa kumtembelea Mzee Maulidi Juma kutoka kwa rafiki yangu miaka na mikaka, Hassan Muchai bin Chui.

Kanidokezea kama mzaha kwamba anataka kuwahamasisha wadau kumtembelea mzee wetu Maulidi Juma kwake Mombasa.

Papo kwa papo akanitumia kwa njia ya ‘wazapu’ baadhi ya nyimbo tamutamu za Maulidi.

Punde si punde, zikaanza harakati za kuchangisha hela kwa ajili ya mzee wetu huku Abdul Noor akiwa ndiye mpokeaji mwaminifu wa michango. Abdul aliaminishwa akajiaminisha.

Tokea hela kidogo, na kidogo kidogo hujaza kibaba, zikapatikana angaa hela za kumzawidi mzee wetu. Safari zikapangwa. Wadau wa Kiswahili toka pembe mbalimbali wakafunga safari kuelekea Mombasa kumsabahi mzee Maulidi Juma ambaye tangu hapo kaacha nyayo zake katika safu ya watribu mahiri.

Mimi mwenyewe nilitamani nijiunge na rubaa ya wenzangu wadau walioelekea pwani. Nakumbuka sana Mwalimu Henry Indindi alinipigia simu na kunirai niandamane nao, ila nilitingwa nikawa siwezi kwenda. Badala yake nilituma mchango wangu kiduchu na salamu kwa Mzee Maulidi.

Ilikuwa furaha ilioje kuona kupitia wazapu na kwenye vyombo vikuu vya habari kama runinga na gazeti letu azizi la Taifa Leo mafanikio ya hafla ya kumuenzi Mzee Maulidi Juma!

Siye ambao hatukuwahi kwenda Mombasa tulibaki kuuma vyanda na kuwahusudu wenzetu waliowahi. Niliona kwamba hata wenzetu wa ughaibuni kama Bi Racheal Maina aliyeko Marekani, naye kapitwa na yaliyojiri Mombasa. Ila kubwa ni kwamba naye kaonesha ukarimu wake kwa kutoa mchango japo katiti kwa ajili ya manju wetu.

Kwa kweli nahisi nimefarijika kwa roho ya insafu walioidhihirisha dhahiri wakereketwa wa Kiswahili. Wamenikumbusha ziara niliiongoza kwenda kumwona marehemu Mzee Hassan Mwalimu Mbega, nilipokuwa mkuu wa kitengo cha Kiswahili katika Nation Broadcasting Division (NBD) mwaka wa 2003. Baadaye hata rubaa kubwa zaidi ilielekea Masinga kumwona Mzee Mbega nikiwa nipo ughaibuni. Waliokwenda kumwona kwenye safari hii walisema alitangaza wazi kwamba hawataweza kumwona tena. Na kweli baadaye mzee wa watu akaenda zake katika njia ya marahaba muda mfupi baadaye.

Ninachosema ni kwamba “Waswahili” wameonyesha utu wa kupigiwa mfano kwa kumuenzi Maulidi Juma, shujaa wa sanaa ya taarab ambaye katelekezwa kama wanavyotelekezwa mashujaa wote janibu hizi za dunia. Hivi karibuni tumesoma habari za mwanariadha Charles Asati aliyekuwa kwenye kikosi cha wanariadha wa kupokezana kijiti walioishindia Kenya dhahabu kwenye mashindano ya Olimpiki 1972. Katika washiriki wote wane, yeye pekee yake ndiye aliyesalia na kwa kweli katupwa katika kaburi la sahau.

Naam, kwa mara nyingine tena “Waswahili” wamethibitisha kwamba utengano ni udhaifu na umoja ni nguvu. Daima tukumbuke tunajenga nyumba moja, tusipiganie fito. Hongereni kwa kumkumbuka Mzee Maulidi Juma.