KINA CHA FIKIRA: Wazazi watie bidii kuwalinda watoto wao sasa

KINA CHA FIKIRA: Wazazi watie bidii kuwalinda watoto wao sasa

Na WALLAH BIN WALLAH

WAKATI umewadia tena wa kuzifunga shule nchini kote ili wanafunzi waende likizoni japo kwa siku chache wakakae na wazazi wao majumbani wapate fursa na satua kupumzisha bongo zao!

Ni matumaini yetu kwamba wazazi watawajibika zaidi kuwatunza na kuwalinda watoto wao wawe salama salmini mpaka siku watakaporejea shuleni kuanza muhula mwingine!

Tunasikitika kuwa shule zitafungwa wakati huu ambapo hali inayumbayumba kutokana na kukithiri kwa visa vya utundu na utovu wa usalama kwa watoto kupotea ama kutekwa nyara! Hiki ni kizungumkuti na kitendawili ambacho hakijateguliwa tujue ni akina nani wanaowateka nyara watoto pindi wanapotoka majumbani au shuleni na wanapotumwa madukani ama wanapoenda kucheza na wenzao?

Sasa tusinyamaze tena! Tuambizane ukweli ulio kweli! Tuache ukweli wa uongo! Tuyafumbue macho tuyaone yasiyoonekana!

Tukishindwa kuona mchana kwenye mwangaza jua linapowaka, tutaonaje katika giza totoro la usiku? Tuache kusikiliza hamrere tu kwamba watoto wanapotea shelabela kisha tunanyamaza hivyo tu! Kwa nini?

Ukweli ni kwamba mambo hayaendi sawa! Chambilecho hayati Profesa Chinua Achebe, “Hamkani si shwari tena!” Siku hizi badala ya kila mja kutimiza wajibu wake kuhusu malezi, ulinzi na usalama wa raia, hasa watoto, watu wamekuwa kiguu na njia kuamini na kuthamini pesa tu.

Tubadilike tuokoe nchi yetu! Tuwakomboe watoto wa taifa hili! Ukombozi huanzia ndani ya mtu binafsi. Tujikomboe tuyakomboe mawazo yetu ili tuikomboe jamii katika taifa letu, hasa watoto!

Enyi walimu wapendwa mliobebeshwa majukumu mazito ya kukaa na wanafunzi kwa muda mrefu zaidi huko shuleni, semeni na watoto hao vijana wetu kuwanasihi na kuwatahadharisha wasimwamini mtu yeyote njiani au mahali popote!

Wambieni, “Mwanafunzi asitembee peke yake kokote kule akienda au akitoka shuleni!”

Wasikubali kulaghaiwa kuenda kununuliwa peremende au lawalawa au chipsi ama kupewa pesa kama chambo! Wawe macho watumie akili tambuzi kila wakati!

Tafadhali wazazi wapendwa, msiache kuwalinda na kuwatunza watoto kwa malezi mema ya kuwapa mahitaji yao ya kila siku; na kuwashauri kila mara badala ya kuwaacha tu mkienda kutafuta pesa! Kwani mnaabudu pesa? Hamjui kuwa kulea mimba si kazi ila kazi ni kumlea mwana?

Ndugu wapenzi, hasa wadau wenye mamlaka ya kulinda usalama nchini, msiyaache maisha ya watoto wetu yawe kama ya watoto wa samaki ambao wakiwa ndani ya maji wanaliwa na samaki wakubwa! Wakitoka nje kando kando ya maji, wanaliwa na ndege waitwao korongo!

Watoto wataishi vipi? Na watatembelea wapi?

wallahbinwallah@gmail.com

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Neema Salome Sulubu

Sifuna asema Rais Kenyatta hahitaji kuunganisha vinara wa...