KINA CHA FIKRA: Daima Magufuli atakumbukwa kwa uzalendo na utetezi wake wa Kiswahili

KINA CHA FIKRA: Daima Magufuli atakumbukwa kwa uzalendo na utetezi wake wa Kiswahili

Na WALLAH BIN WALLAH

KIONGOZI yeyote awaye mwanamapinduzi na mzalendo halisia mara nyingi hukumbatia na kuonea fahari lugha ya taifa lake!

Anajua dhahiri shahiri kwamba lugha ya taifa ndicho chombo muhimu cha kuleta umoja na mshikamano wa kweli nchini.

Katika mataifa yetu ya Afrika Mashariki, hasa Kenya na Tanzania, tunajivunia lugha ya Kiswahili kwa kutuunganisha! Hapo ndipo ninapochukua fursa hii katika kauli ya leo kumtaja kwa heshima na taadhima hayati Rais Dkt John Pombe Magufuli kwamba alisimama kidete bila kutetereka kuitetea lugha ya Kiswahili nchini Tanzania kila mahali na kila siku wakati wote wa uongozi wake hadi mauti yalipochukua roho yake iliyopenda Kiswahili kupeleka mapumzikoni mbele ya Mwenyezi Mungu!

Wakati tunapomwombea Rais mpendwa wetu Dkt John Pombe Magufuli Mwenyezi Mungu kuilaza roho yake mahali pema peponi, tumpongeze kwa dhati kwa jukumu kubwa na uzalendo wake wa kukitukuza, kukikuza na kukitumia Kiswahili katika hotuba na hafla zake zote za uongozi, kisiasa, kiuchumi, kitaifa na kimataifa! Rais mpenda watu na nchi yake, mzalendo mchapakazi, John Joseph Pombe Magufuli ametuachia mfano mwema sana ambao endapo hatukuiga alipokuwa hai, tuige sasa na tuendeleze mikakati na harakati za kumheshimu na kumuenzi daima Mwana huyu wa Afrika, mzalendo ambaye hakuyumbishwa wala kubabaishwa na kasumba za kikoloni! Tumpe heko kwa juhudi zake za kuipenyeza lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Angola, Botswana, Ethiopia na kwenye Muungano wa nchi za Afrika Kusini. Buriani mtetezi wa Kiswahili, Rais John Joseph Magufuli! Mola ailaze roho yako mahali pema pa watu wema peponi! Amina!!

Ndugu wapenzi, watu waliotenda matendo mema duniani wanapoondoka, matendo yao mema hudumu daima katika nyoyo za walio hai! Nasi tuyakumbuke mawazo mema ya kiongozi huyu ya kukikuza Kiswahili! Aidha, tuwapongeze zaidi wadau wa Kiswahili waliowahi kumtuza Rais John Magufuli tuzo adhimu ya Kiswahili katika Kongamano lililoandaliwa Chuo Kikuu cha Dodoma mwanzo wa mwaka huu.

Ni matumaini yangu kwamba Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan atakitetea na kukiendeleza Kiswahili kama hayati Rais John Magufuli! Ninavyomjua Mama Samia Suluhu pia mzalendo kindakindaki mpenda Kiswahili. Mliohudhuria Kongamano la BAKIZA mwaka 2018 katika ukumbi wa Abdul Wakil, Zanzibar, bila shaka mnakumbuka nilimtuza medali ya dhahabu ya Tuzo za Wasta kwa Ufasaha na Umilisi wa Kiswahili.

Wakati tunapomhimiza Mama Samia afuate nyayo za kukitukuza Kiswahili, kwa majonzi na simanzi tunasema, buriani Rais mpendwa Dkt John Magufuli mtetezi wa Kiswahili!!!!

You can share this post!

NASAHA: Hakikisho la kufanya vizuri ndicho kichocheo kwa...

Maelfu katika hatari ya kufa kwa corona