KINA CHA FIKRA: Profesa Ken Walibora alikichapukia Kiswahili kwa kauli na matendo, Mola azidi kumrehemu

KINA CHA FIKRA: Profesa Ken Walibora alikichapukia Kiswahili kwa kauli na matendo, Mola azidi kumrehemu

Na WALLAH BIN WALLAH

LEO tumeumega mwaka mzima kasoro siku tatu tangu alipoaga dunia Profesa Ken Walibora mwandishi mahiri mtajika wa vitabu vya Kiswahili aliyetuacha tarehe kumi Aprili, 2020.

Katika kitabu cha Juliasi Kaizari kilichotafsiriwa na Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Mark Antonio anasema, “Ndugu Warumi, matendo mema ya mwanadamu huishi milele baada ya mwanadamu kuondoka duniani! Kwa hivyo, mimi nimekuja hapa kumzika Kaizari wala sikuja kumsifu Kaizari, kwa sababu nyinyi nyote mnaelewa matendo mema ambayo Kaizari aliwatendea Warumi wote!”

Katika uzi huo huo, ninaunganisha kwa kusema kwamba, mimi siandiki makala haya ya leo kumsifia hayati Ken Walibora, ila nimeshika kalamu na kuupinda mgongo wangu kuandika kumkumbuka Ndugu Profesa Ken Walibora mwandishi mwenzetu aliyetuacha duniani tukigwayagwaya kwa majonzi na machozi baada ya kutuondoka ghafla tarehe kumi mwezi wa nne mwaka jana! Sina maneno mapya ya kumsifia hayati Ken Walibora katika makala haya kwa sababu kazi alizofanya katika kukuza Kiswahili pamoja na vitabu alivyoviandika matopa kwa matopa, vinatosha kutangaza sifa zake kwa matangazo ya kweli bila matilia chumvi milele na milele duniani! Ndipo kila mara tunakumbushana kwamba ukiwa hai duniani, tenda matendo mema watu wayaone!

Matendo ni muhimu kuliko maneno matupu! Matendo hayafi hata kama mtu mwenye matendo ameondoka duniani! Tenda matendo uyaache duniani! Usiishi bila matendo! Utakuwa sawa na kalamu isiyokuwa na wino iliyoandika bila kuacha maandishi!

Jitahidi uwe kama mdudu konokono ambaye huacha alama kila mahali anapopitia bila kufutika! Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno! Tenda watu wayaone matendo ili nawe ukumbukwe kwa matendo si kwa maneno matupu!

Aidha sitaki kujivisha joho la kumsifia sana hayati Profesa Ken Walibora kwa sababu watu wote waliobahatika kukutana naye, wanaelewa fika kwamba Komredi Ken Walibora alikuwa mtu wa watu, mcheshi mwenye uso wa bashasha siku zote; mwungwana mwenye roho safi asiyejua kununa anaponena maneno yake ya busara!

Alicheka na kila mtu na kumheshimu kila mja! Hatuwezi kumsahau mzalendo huyu mpenzi wa Kiswahili aliyeitetea lugha yetu adhimu kwa udi na uvumba hadi siku ya mauko yake!

Ndugu wapenzi, namalizia kauli ya leo kwa kukariri kwamba, mtu ni matendo! Ukiwa mwema utende mema duniani uache matendo mema! Bado tunamkumbuka Ndugu Profesa hayati Ken Walibora mwandishi mtajika wa Kiswahili kwa matendo yake na kazi zake bora kama jina lake Walibora! Mola aisitiri roho yake mahali pema peponi! Aamina!!!!

You can share this post!

China yatoa mchango muhimu kupunguza umaskini duniani

Ajali ya mabasi mawili Kwa Shume yasababisha vifo vya si...