CECIL ODONGO: Kina mama wajitokeze na kusaka kura bila kutegemea vya bwerere

CECIL ODONGO: Kina mama wajitokeze na kusaka kura bila kutegemea vya bwerere

CECIL ODONGO

HATUA ya viongozi wengi wa kike kujitokeza kupambana na wanaume au hata wanawake wenzao kuwania kiti gha ugavana katika kaunti mbalimbali inaonyesha mwamko mpya wa kisiasa nchini na itatokomeza dhana kuwa wanawake hutegemea tu nafasi za uteuzi wa vyama.

Tangu kurasimishwa kwa katiba mpya mnamo 2010, idadi ya wanawake wanaoshikilia nyadhifa za uongozi imekuwa ikiongezeka na inaonyesha kuwa, juhudi za kuhakikisha wanawake wanashikilia angalau theluthi moja ya nafasi hizo hatimaye itatimia hivi karibuni.

Kati ya viongozi wote 1883 waliochaguliwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, wanawake walikuwa 172 ikilinganishwa na 145 baada ya uchaguzi mkuu wa 2013.

Wanawake walioteuliwa katika mabunge ya kaunti ni 650, seneti walikuwa 18 huku katika Bunge la Kitaifa wakiwa sita.

Hata hivyo, huenda hali ikabadilika katika uchaguzi mkuu ujao na idadi ya wanawake waliochaguliwa kupanda kwa kuwa wengi wamejitosa siasani kuwania viti vya udiwani, ubunge, useneta, ugavana na nafasi ya mbunge mwakilishi wa kike kwenye kaunti zote 47.

Ingawa hivyo, kuna matarajio tele kuwa kiti cha gavana ambacho kinahusudiwa mno kwa kuwa kinaambatana na kusimamia bajeti ya mabilioni ya fedha, kitakuwa kinashikiliwa na angalau zaidi ya wanawake watatu kuliko ilivyo kwa sasa kutokana na baadhi ya wanasiasa vigogo wa kike kuamua kujibwaga ulingoni.

Kwa sasa ni Charity Ngilu (Kitui), Anne Waiguru ( Kirinyaga) na Anne Kananu ( Nairobi) ambao ndio magavana wa kike.

Katika kaunti ya Kirinyaga, ni wazi kuwa wanaume wamepigwa kumbo katika mbio hizo na huenda gavana akawa Bi Waiguru au Purity Ngirici wanaopigania tiketi ya UDA.

Vivyo, hivyo itakuwa kibarua kigumu kumbandua Bi Ngilu katika Kaunti ya Kitui kutokana na rekodi yake nzuri ya maendeleo katika muhula wa kwanza wa uongozi wake.

Susan Kihika (Nakuru), Cecily Mbarire (Embu), Faith Gitau (Nyandarua) na Soipan Tuya (Narok) nao wana nafasi nzuri iwapo mwishowe watashinda mchujo na kupata tiketi za UDA.

Hali ni hiyo hiyo kwa Gladys Wanga na Wavinya Ndeti wakitwaa tiketi za ODM na Wiper kupambania ugavana Homa Bay na Machakos mtawalia.

Hata hivyo, changamoto kubwa kwa wanawake hawa ni kuwa, azma yao inapingwa na viongozi wenzao wa kike kwenye baadhi ya kaunti.

Hii inaadhihirisha kuwa adui ya mwanamke ni mwanamke na hilo linaweza kuchangia kubwagwa kwao.

Mfano mzuri ni katika kaunti ya Homa Bay ambapo wabunge Lillian Gogo (Rangwe) na Millie Odhiambo (Homa Bay) wamekuwa wakiendesha kampeni kali dhidi ya Bi Wanga ndani ya ODM.

  • Tags

You can share this post!

Mama mboga ‘aoza’ binti kwa mteja wa kila siku

Vipusa wa Uingereza waweka rekodi mpya ya ufungaji mabao...

T L