Kinadada wa Kenya wafundisha wenzao kutoka Uganda jinsi ya kusakata mpira wa magongo

Kinadada wa Kenya wafundisha wenzao kutoka Uganda jinsi ya kusakata mpira wa magongo

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya mpira wa magongo ya wanawake ya Kenya imeaibisha Uganda 11-0 katika mechi ya kimataifa uwanjani Sikh Union Nairobi, Alhamisi.

Wakenya walizamisha majirani hao wao kupitia magoli ya

Grace Okumu (matatu), Gilly Okumu (mawili), Naomi Kemunto (mawili) nao Flavian Mutiva, Caroline Guchu na nahodha Tracy Karanja wakachangia bao moja kila mmoja.

Timu ya wanaume ya Kenya nayo ilitupa uongozi wa bao moja ikitoka 1-1 dhidi ya timu ya Uganda ya wanaume iliyopigiwa ugani humo baadaye Alhamisi.

Katika kitengo cha kinadada, Kenya ilidhibiti mchezo katika idara zote ikinyakua robo ya kwanza 3-0 kupitia mabao ya Gilly dakika ya sita, Grace dakika moja baadaye na Kemunto dakika ya 13.

Hakuna aliyepata bao katika robo ya pili kabla ya Kenya kupata makali yake tena katika robo ya tatu baada ya mapumziko ilipochana nyavu za Uganda kupitia kwa Gilly, Grace na Kemunto.

Chipukizi Grace alikamilisha mabao yake matatu dakika 12 kabla ya kipenga cha mwisho kilie, huku wachezaji wazoefu Mutiva, Guchu na Karanja wakipata goli moja kila mmoja katika ushindi huo mkubwa.

Kenya na Uganda zinatumia mechi hizo ambazo zitaendelea Machi 20 na Machi 21 kujiandaa kwa Kombe la Afrika litakaloandaliwa mwezi Januari 2022 nchini Ghana.

Majirani hawa walifuzu kushiriki dimba hilo kutoka mashindano ya Kaskazini-Mashariki bila kutokwa jasho baada ya wapinzani wengine kukosa kujiandikisha.

  • Tags

You can share this post!

Ndoto ya wanatenisi ya mezani wa Kenya kuwa Olimpiki yazimwa

Kenya ilipoteza Sh560 billioni kutokana na corona 2020 –...