Michezo

Kinara wa Ingwe apongeza timu kwa bao moja dhidi ya Vihiga

July 31st, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa AFC Leopards Dan Mule amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kufuatia ushindi walioutwaa dhidi ya Vihiga United FC katika uwanja wa Mumias Sports Complex Agosti 29.

Ushindi huo ulipatikana kupitia bao la kiungo Marvin Nabwire katika kipindi cha kwanza na ulijiri baada ya kichapo cha 2-1 mikononi mwa Mabingwa watetezi Gor Mahia kwenye debi ya Mashemeji Agosti 23.

Kando na kutoa pongezi yake kuhusu matokeo hayo dhidi ya timu inayonolewa na kocha msifika Mike Mururi, Mule amewataka wanadimba hao wajikakamue na kushinda nyingi za mechi zilizosalia ili wamalize ligi katika mduara wa tatu bora.

“Ningependa kuwapongeza wachezaji kufuatia ushindi dhidi ya Vihiga United. Walicheza vizuri na nawaomba waendelee kutia bidii ili kushinda nyingi za mechi zilizobaki,”  akasema Bw Mule.

“Tukishinda mechi yetu ijayo tutatinga nafasi ya pili. Tunafaa kupunguza mwanya wa alama kati yetu na mahasimu Gor Mahia ndipo tumalize k ndani ya mduara wa timu tatu bora,” akaongeza Bw Mule.

Ingwe watacheza dhidi ya Simba SC kutoka Tanzania Agosti 8 katika mechi za kuadhimisha siku ya kubuniwa kwa mabingwa hao wa ligi ya Vodacom nchini Tanzania.

“Itakuwa mechi nzuri kwa vijana wetu haswa kwa wale ambao wamekuwa wakisugua benchi,” akasema Mule.

Ingwe watawajibikia ligi Agosti 5 kwa kutesa dhidi ya Mathare United katika uga wa Kenyatta mjini Machakos.