Habari Mseto

Kinara wa kampuni ya bima akana kuiba mamilioni

September 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA mkuu wa kampuni ya bima alishtakiwa Alhamisi kwa wizi wa zaidi ya Sh11.8milioni anazodaiwa alizipokea kwa niaba ya kampuni nyingine nne.

Bi Cecilia Bridgit Rague, kinara wa kampuni ya Underwriting Insurance Brokers alikana shtaka mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku.

Kiongozi wa mashtaka Anderson Gikund alieleza mahakama Cecilia alitekeleza wizi huo mnamo Desemba 12 2019 katika jengo la NCBA iliyoko Westlands Nairobi.

Hakimu alifahamishwa mshtakiwa alipokea pesa hizo mali ya Sanlam General Insurance Limited.

Korti ilijuzwa pesa hizo zilikuwa zipelekewe makampuni ya Bima ya Waica, Continental, Ghana na CICA Reinsurance.

Mshtakiwa aliyejitetea mahakamani aliomba hakimu amwachilie kwa dhamana.

Bw Gikunda hakupinga ombi hilo ila aliomba mahakama izingatie kiwango cha pesa anachodaiwa kaiba kinara huyo wa kampuni ya bima.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu.

Kesi itaanza kusikizwa Desemba 10,2020.

Hakimu aliamuru mshtakiwa akabidhiwe nakala za mashahidi aandae ushahidi wake wa kujitetea.