Habari

Kinara wa KQ alipwa Sh62m shirika likipata hasara ya mabilioni

May 22nd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

AFISA mkuu mtendaji  wa shirika la ndege la Kenya Airways Sebastian Mikosz anasemekana kulipwa jumla ya Sh62.89 milioni mwaka 2018 licha ya shirika hilo kuendelea kupata hasara.

Hii ni kumaanisha kwa mwezi alikuwa akilipwa Sh5.2 milioni. Kwa jumla, alilipwa mshahara wa Sh42 milioni, marupurupu ya Sh16.4 milioni na marupurupu mengine yasiyohusisha fedha ya thamani ya Sh4.44 milioni.

Raia huyo wa Poland aliajiriwa Juni 2017 kwa lengo la kuisaidia KQ kuimarika tena baada ya msururu wa hasara. Mwaka 2018, kampuni hiyo ilipata hasara ya Sh7.5 bilioni baada ya ushuru, ikilinganishwa na Sh6.4 bilioni mwaka uliotangulia.

Kampuni zilizoorodheshwa katika soko la hisa zinafaa kuweka wazi mshahara na marupurupu kwa maafisa wakuu kwa kumujibu wa sheria.

Mkurugenzi huyo alilipwa Sh46.69 mwaka wa 2017 baada ya kufanya kazi kwa miezi saba pekee, kumaanisha alilipwa Sh6.67 milioni kwa mwezi.

Mshahara ulikuwa ni Sh24.63 milioni, marupurupu yalikuwa ni Sh18.6 milioni na marupurupu yasiyohusisha fedha yalikuwa ni Sh3.4 milioni.

Hii ni kumaanisha kuwa malipo yake ya jumla yalipungua 2018 ikilinganishwa na 2017.

Katika kipindi kilichokamilika Desemba 31, 2018, mwenyekiti wa KQ Michael Joseph, ambaye anaondoka mwaka huu alilipwa Sh18 milioni ikilinganishwa na Sh13.5 milioni 2017.

Shirika hilo linaendelea kupata hasara licha ya mikakati iliyowekwa kuliimarisha, ambayo kufikia sasa haijazaa matunda yoyote.