Habari Mseto

Kinara wa Team Kenya michezo ya Olimpiki 2016 ajitetea mahakamani

July 30th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KINARA wa timu ya Kenya iliyoshiriki katika michezo ya Olimpiki ya 2016 iliyofanyika Rio De Janeiro nchini Brazil 2016 Stephen Soi alisema Jumatano hakuhusika na ubadhirifu na kashfa ya Sh88 milioni iliyokumba michezo hiyo huku akikiri hajarudishia Rais Uhuru Kenyatta bendera ya Kenya aliyomkabidhi kuongoza kikosi kilichoshinda medali sita za dhahabu.

“Nchi hii ilinyakua medali nyingi zaidi za dhahabu kuliko michezo ingine ya Olimpiki tangu mwaka wa 1964,” Bw Soi aliambia mahakama inayoamua kesi za ufisadi.

Bw Soi alimweleza hakimu mkuu Bi Elizabeth Juma kwamba badala ya kupokewa kwa heshima “alilakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na maafisa wa polisi kama mhalifu.”

“Hadi wa leo sijawahi rudisha bendera ya Kenya niliyopewa na Rais Kenyatta. Siku moja nitairudisha tu,” alisema Soi.

Kiongozi huyo wa wanariadha waliopeperusha bendera ya nchi hii katika michezo hiyo ya Rio alidokeza kwamba Kenya ilinyakua jumla ya medali 13, sita za dhahabu, sita za fedha na moja ya shaba.

“Nilitarajia kupokewa kwa taadhima jinsi mjomba wangu Kipsoi arap Belsoi alivyolakiwa kwa heshima na hayati Mzee Jomo Kenyatta baada ya kuletea nchj hii heshima wakati wa michezo ya Olimpik ya miaka ya 1964, 1968 na 19272,” Bw Soi alisema mahakamani alipoanza kujitetea katika kesi inayowakabili pamoja na aliyekuwa Waziri wa Michezo Hassan Wario na aliyekuwa Katibu mkuu wizara hiyo hiyo Titus Ekai.

Huku akipandwa na hasira kali, Bw Soi alimlaumu afisa aliyechunguza kesi hiyo Inspekta Mkuu Mike Muia aliyedai hakutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Stephen Soi (kushoto) abembelezwa na mkewe na pia wakili Kimutai Bosek katika mahakama ya Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Ilibidi mahakama isimamishe kesi atulie huku mkewe akienda kumtuliza kizimbani.

“Naomba muda nitulie. Nahisi hasira kali. Nahitaji dakika kadhaa nitulie,” Soi alimsihi hakimu.

“Mimi sikuhusika kamwe na malipo ya fedha ama kuwapatia mashambiki walioandamana na  Team Kenya hadi Rio.Waliohusika na malipo ni wakuu wa kamati ya Olimpik (Nock) walioongozwa na Dkt Kipchoge Keino na aliyekuwa katibu mkuu wa Nock Francis K Paul,” alisema Bw Soi.

Mshtakiwa huyo ambaye alistaafu kutoka Idara ya Polisi alisema , “ Nilitoa mafunzo mema kwa makrutu wa Polisi Kiganjo na wala sikuwafundisha kutekeleza majukumu yao vibaya jinsi nilitendewa na Insp Muia,” alisema Bw Soi  huku “akitaka hakimu amfukuze kutoka kortini afisa huyo wa Polisi.”

Alisema Bw Soi, “kila ninapomwona Insp Muia kortini ninakumbuka dhuluma niliyotendewa nikihojiwa. Hakutekeleza kazi yake ipasavyo. Naomba hii mahakama imfukuze kabisa kutoka kwenye kesi hii kwa vile alitoa habari za kupotosha akitoa ushahidi.”

Bw Soi alisema Inspekta Muia alidai kortini kikosi cha Kenya kilikaa kwenye hoteli ya kifahari yenye vitanda 125 lakini “hakujua kikosi cha Kenya kilikuwa kikiishi katika makazi maalum almaarufu ‘Olympics Village’.”

Makazi haya huwa nyumba maalum zilizojengwa kuishi wanamichezo na wala sio hoteli.

“Mimi sikuwa ajenti wa kununulia wanariadha na mashabiki tikiti za ndege. Mashtaka ninayodaiwa nilihusika na tikiti hayana msingi na hii korti yafaa kuyafutupilia mbali,” Soi alijitetea.

Soi, Wario, Ekai aliyekuwa ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Urusi, na Paul; wanajitetea katika kashfa ya Rio ambapo mamilioni ya pesa zilipotea.

Soi alisema ikiwa kuna yeyote anayeweza kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa pesa zilizotengewa wanamichezo ni mwekahazina Bi Fridah Hilda aliyegeuzwa kuwa shahidi badala ya mshtakiwa.

Soi alisema kashfa hiyo ikitendeka alikuwa amesafiri hadi Rio na “hakuwa nchini. Sikuwa nafanya kazi kwa Wizara ya Michezo na wala sikuhusika na masuala ya fedha kwa njia yoyote ile.”

Kesi iliahirishwa hadi Agosti 17 baada ya mmoja wa viongozi wa mashtaka kupata maradhi ya Covid-19.