Michezo

Kinara wa Zamalek asema Gor ni timu dhaifu

February 20th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

RAIS wa vigogo wa soka kutoka Misri, Mortada Mansour amesema kwamba mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) Gor Mahia ni timu dhaifu na haelewi jinsi ilvyoshinda timu yake 4-2 katika mechi ya makundi ya Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).

Mansour vile vile alimkashifu kocha wa Zamalek Christian Gross kama ‘mkufunzi kichwa ngumu’ na ameshindwa hadi leo kumwelewa anafanya kazi kivipi huku akisema matamshi yake hayalengi kumgonganisha kocha huyo na mashabiki wa Zamalek.

Matamshi ya Afisa huyo wa timu yanajiri baada ya Zamalek kupoteza nafasi ya kutwaa uongozi wa kundi D kwa kuruhusu NA Hussein Dey ya Algeria kusawazisha bao dakika ya mwisho kwenye mechi ya CAF katika uwanja wa Borg El Arab Februari 13, 2019.

“Gross ni kichwa ngumu na hawezi kutueleza chochote kuhusu matokeo mabaya ya timu. Sitaki kumgonganisha na mashabiki wetu lakini lazima niseme kwamba sikufurahishwa na sare dhidi ya NA Hussein Dey iliyotuponza nafasi ya kupanda hadi nafasi ya kwanza kundini,”

“Juzi tulibanduliwa kwenye kiny’ang’anyiro ya Kombe la Waarabu na timu ya Ittihad, na wiki jana tulipoteza mechi dhidi ya mpinzani dhaifu kutoka Kenya (Gor Mahia). Haya mambo ni magumu kuyaelewa,” akasema Mortada kupitia mtandao wa klabu hiyo.

Zamalek wanaburura mkia kwenye kundi D linalojumuisha Gor Mahia(nafasi ya tatu), Na Hussein Dey (nafasi ya kwanza) na Petro de Luanda (nafasi ya pili).