Kinara wa zamani wa EACC akana kuhusika katika sakata ya Kemsa

Kinara wa zamani wa EACC akana kuhusika katika sakata ya Kemsa

CHARLES WASONGA na SAMUEL OWINO

ALIYEKUWA Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Halakhe Waqo akana kuhusika katika sakata ya ununuzi wa bidhaa za corona ya thamani ya Sh7.8 bilioni katika Mamlaka ya Dawa Nchini (Kemsa).

Akiongea Ijumaa alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) Bw Halakhe hata hivyo alikubali kuwa alimdhamini mmoja wa wawasilishaji wa bidhaa katika mamlaka hiyo alipotaka kukosa fedha kutoka benki moja ya humu nchini.

Bw Waqo alisisitiza kuwa hajawahi kupewa zabuni ya kuuzia Kemsa bidhaa zozote wala kuwa mkurugenzi wa mojawapo ya kampuni 107 zilipata zabuni ya kuiuzia bidhaa za kupambana na Janga la Covid-19.

“Sijawahi kuomba zabuni kuuza bidhaa za kudhibiti corona kwa Kemsa, kama mtu binafsi au kupitia kampuni fulani. Sikuhusishwa katika upatikanaji wa vibali vya kuuza bidhaa hizo,” akasema alipofika mbele ya kamati hiyo katika majengo ya bunge, Nairobi.

Bw Waqo aliwaambia wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, kwamba alimsimamia kampuni ya Aszure Commercial Services kama mdhamini katika Benki ya First Communty ili iweze kupata mkopo iweze kuwasilisha bidhaa za thamani ya Sh347 milioni kwa Kemsa.

“Mimi sio mwenye hisa au mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Aszure Commercial Services,” akasema.

“Nilikuwa ajenti wa ufadhili kwa kampuni hiyo iliyopewa zabuni na Kemsa iiuzie bidhaa za kuzuia msambao wa virusi vya corona,” Waqo akaongeza.

Alieleza kuwa kampuni hiyo ilijulishwa kwake na afisa mmoja wa benki hiyo katika wiki ya mwisho ya Aprili, 2020.

“Kwa sababu niko na akaunti katika benki ya First Community, mmoja wa wakurugenzi wa Aszure Commercial Services aliniomba niwe mdhamini wao kwa mkopo waliotaka kutoka kwa benki hiyo,” akasema Bw Waqo.

Mapema mwezi huu mkurugenzi mmoja wa Aszure Commercial Services Bi Zubeda Nyamlondo aliambia kamati hiyo ya PIC kuwa alisaidiwa na Waqo kupata mkopo kutoka benki ulimsaidia kuwasilisha barakoa 500,000 aina ya N95.

You can share this post!

Naibu Gavana wa Kericho Susan Kikwai afariki kutokana na...

Ajowi na Akinyi wateuliwa kushiriki ndondi Olimpiki