Habari Mseto

Kinara wa zamani wa KPC abambwe – Mahakama

December 10th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mkurugenzi mkuu wa shirika la kusambaza mafuta nchini (KPC) Bw Charles Kiprotich Tanui ameamriwa atiwe nguvuni kwa ufujaji wa zaidi ya Sh644 milioni za umma.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti aliamuru Bw Tanui atiwe nguvuni pamoja na washukiwa wengine 10 walioshtakiwa kwa ufujaji wa Dola za Marekani 6,441,700 (Sh644milioni)  za ununuzi wa mitambo na mabomba ya kusambaza mafuta.

Bw Ogoti aliamuru 11 hao washikwe na kufikishwa kortini Januari 22 2019.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kuwa 11 walikuwa wameamriwa wafike katika afisi za tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuhojiwa na kufunguliwa mashtaka.

Kwa jumla EACC ilikuwa imewaagiza washukiwa 18 wanaowajumuisha wafanyakazi wa wa KPC na wafanyabiashara.

Mawakili Michael Muchemi (kushoto) , Felix Kiprono na Muthomi Thiankolu wanaowatetea washtakiwa. Picha/ Richard Munguti

Waliojisalamisha kwa maafisa wa EACC kuandikisha taarifa na hatimaye wakashtakiwa ni Francis Githaiga Muraya,  Samuel Odoyo Mikwa, Nicholas Gatobu , Peter Gaitho Machua, Jane Jesanai Nakodony , Charles Nderitu Maitai na Emilio Mwai Nderitu.

Walishtakiwa kati ya Oktoba 2014 na Julai 2015 wakiwa waajiriwa wa KPC na wafanyabiashara walifanya njama za kuilaghai shirika hilo Dola za Marekani 6,441,700.40 (sawa na Sh644,700,000) katika mradi wa kununua mitambo ya kusambaza mafuta na mabomba.

Kandarasi ya kununua mitambo na mabomba hayo inajulikana kwa jina Aero Dispenser Valves Limited.

Afisa anayechunguza kesi hiyo aliamriwa awape nakala za ushahidi washtakiwa hao saba kabla ya Janauri 22 2019 kesi itakapotajwa.

Kiongozi wa mashtaka Bi Carol Kimiri. Picha/ Richard Munguti

Awali mameneja hao wakuu saba wa KPC Walijisalamisha kwa polisi na kushtakiwa katika awamu ya pili ya kuchukuliwa hatua kwa wafanyakazi wa shirika hilo waliohusika na ufisadi uliogharimu walipa ushuru zaidi ya Sh61bilioni.

EACC ilisema kwamba saba hao walikamatwa kufuatia uporaji wa zaidi ya Sh600 milioni katika kampuni hiyo wakati wa ununuzi wa mitambo 58 ya kuwekwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Oktoba 2014.

EACC ilisema kwamba inawasaka washukiwa wengine tisa akiwemo Bw Tanui, wakurugenzi wawili wa kampuni ya Aero Dispenser Valve Ltd, huku serikali ya Kenya ikawasiliana na ya Canada ichunguze na kuwafungulia mashtaka mameneja wa kampuni ya Allied Inspection and Testing Inc wakiongozwa na mmiliki wake Jim Yukes.

EACC inamsaka Bw Tanui, meneja wa huduma Philip Kimelu, meneja msimamizi wa stima Bramwell Wanyalika, meneja wa Teknolojia na mawasiliano Francis Muraya, mhandisi wa mitambo Charles Ochieng’ Ouko, mhasibu Emilio Mwai Nderitu, wakurugenzi wawili wa kampuni ya Aero.