Makala

KINAYA: Asiyejisajili kupiga kura asiitamani yangu, huyu Mariga ametuzoea!

September 14th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

NAAM, vile tu Kethi Kilonzo alivyotuzoea kabla ya kufukuziwa mbali na Tume Huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kutokuwa na kura, tukamzika kwenye kaburi la sahau.

Haileti raha kwamba watoto matajiri na wale ambao akina baba zao wanazo tele benki huwachukulia Wakenya wa kawaida kimzaha.

Hawatuheshimu hata kidogo.

Rafiki yangu sikiza: Kwanza usahau msimamo wako wa kisiasa, iwe uko ODM, Jubilee, Wiper au hata kile cha Musalia Mudavadi ambacho sikikumbuki jina.

Kalia jamvi tujadiliane pasi na kufungamana na upande wowote, unisafie nia na kuniambia, ikiwa mtu hajawahi kupiga kura, kwa nini mimi nawe tumpigie?

Kwani sisi ambao tumezoea kurauka vituoni ili kutumbukiza kura zetu kwenye madebe ni wajinga kiasi gani?

Mtu ambaye hajawahi kuamka mapema kama sisi kumchagua mtu mwingine yeyote anataka kura zetu azipeleke wapi?

Aliambiwa na nani kwamba sisi ni mitambo ya kupiga kura tu na wala si kupigiwa? Hapa si heshima imepungua sana mtu wa aina hiyo anaposisitiza tumchague?

Si hata akili zetu zitakuwa zimeyeyuka na kuwa uji ikiwa tutakubali mtu kama huyo awe kwenye karatasi za kura, eti tumchague akatuwakilishe bungeni?

Bibi mzaa mama, kipenzi changu marehemu sasa, akiniambia kuwa mtu asiye na kuku hawezi kupewa jukumu la kuwalinda vifaranga dhidi ya mwewe.

Nikitumia busara za bikizee huyo, hata bila kuangalia Katiba ya Kenya inasema nini kuhusu mwaniaji, sina ugumu wa kuamua kwamba (pengine) Mariga ni ovyo!

Usithubutu kuniambia stakabadhi fulani zinaonyesha alijiandikisha kupiga kura hivi majuzi! Nina shaka na hilo, na hata lingekuwa kweli sitakubali kudharauliwa.

Ikiwa kwa kweli mwanasoka huyo alijiandikisha kupiga kura, dhamira yake ilikuwa kujiweka tayari kuwania ubunge wa Kibra, apigiwe kura yeye na wala si ampigie mtu.

Asingetaka kuwania hangejiandikisha. Hata hatungemsikia akitajwa kuhusiana na siasa; angekuwa akifanya mazoezi ya soka.

Wakati huo makabwela tusio na kazi muhimu tungekuwa tukijikuna vichwa kutafuta mtu wa kuchagua kwa kuwa wenyewe tunajichukia na kujidharau ajabu!

Sheria ingewaruhusu watu wasio na kura kuwania nyadhifa zozote, matajiri wengi hawangejichosha kwenda vituoni kujiandikisha. Wanatuona wajinga sana eti.

Kisa na maana? Mimi nawe ni vyombo vya kuwachagua, kwetu hakuna mbegu za viongozi, tunazaliana wafuasi tu!

Hebu jiulize wakili Kethi Kilonzo, mwana wa marehemu Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo, angekosaje kujiandikisha kupiga kura ilhali babake alihitaji kuchaguliwa?

Nina jawabu sahihi: Mtazamo wa wakili huyo, na bila shaka wa baba yake, ulikuwa kwamba kuna wajinga na malofa wa kutosha.

Kethi hakuhitaji kupigwa na baridi ya asubuhi wala kutunga foleni kumchagua babake, makabwela wapo.

Ni Mutula alipoaga dunia tu ambapo Kethi alijua umuhimu wa kujiandikisha.

Hata Mariga alijua umuhimu wa kujiandikisha pale Ken Okoth, aliyekuwa mbunge wa Kibera, alipoaga.

Hiyo ni tabia mbaya inayonasibishwa na fisi, nguruwe na wanyama wengine wachafu ambao hukimbia kwenye majalala ya takataka kufukua mizoga na makombo yaliyotupwa!

Asiye na kura asiitake yangu, nyege ni kunyegezana.

 

[email protected]

 

MUHIMU KWA MSOMAJI

Hatima ya McDonald Mariga iwapo atagombea kiti uchaguzi mdogo eneobunge la Kibra itabainika Jumatatu ambapo uamuzi wa rufaa aliyokata utatolewa.