Makala

KINAYA: ‘Baba’ hajawaambia Wakamba vizuri ila jinsia zote zina matapeli

November 10th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

‘WEWE una umama sana! Ondoa umama hapa! Una tabia za kike! Unatembeaje kama mwanamke? Mbona umekuwa mdaku kama mwanamke?’

Hayo, na mengine yasiyoandikika, ni baadhi ya matusi ambayo hutemwa pale mwanamume anadhalilishwa. Hayachekeshi, yanaudhi. Hayavutii, yanasinya.

Tusidanganyane! ‘Baba’ hajawaambia Wakamba vizuri. Amewadharau. Amewadunisha. Amewakosea heshima pakubwa. Huo ndio ukweli.

Japo alisema kimzaha kwamba Wakamba ni waaminifu, eti ni sawa na wanawake ambao wakiahidi kutoa vitu hawavunji ahadi, utamaduni wa Mkenya unanipa maana tofauti.

Kila unapomfananisha mwanamume na mwanamke huwa unanuia kumkera dume wa watu, hakika huwa umemwita shoga kiujanja, na unaweza kupigwa kibao!

Wanaojidai watetezi wakuu wa wanawake – au wanaoziramba nyayo za ‘Baba’ – watakuja juu na kusema eti nikome, mwanamke si kiumbe duni wala dhaifu kiasi hicho.

Hata hivyo, mwenzako haunipigi mshipa ninapojadili mambo haya kimasomaso, anayetaka mjadala anijie tuziende. Kila tamko, hata hilo la ‘Baba’, lina misingi ya jamii.

Kwanza tuulizane maswali kadhaa rahisi: Ni wanawake gani hao waaminifu kiasi cha kupigiwa mfano na ‘Baba’? Ni wa Kenya hii au dunia ya kusadikika?

Kwani ‘Baba’ huhusiana na wanawake wepi hao wasiomhadaa? Wanaume tumehadaiwaje dunia hii! Hadaa ingekuwa mjeledi tungejaa madonda miilini!

Tusemezane ukweli: Ni wanaume wangapi ambao hawajawahi kudanganywa, yaani ukamtumia mtu nauli kwa M-pesa aje kwako, kisha ukamsubiri mchana kutwa asije?

Kitambo kidogo ukipandwa na hasira, thubutu umpigie simu tu, unapata keshaizima zamani sana, unaambiwa ‘mteja wa nambari uliyopiga hapatikani kwa sasa’!

Na kwa sababu huna akili timamu wakati mwingine, akiwasha simu kisha akupe visingizio visivyo na mbele wala nyumba, unajitia ukamanda na kumtumia nauli nyingine.

Kwa nini? Eti ile ya mwanzo ililiwa na panya au mbwa, ya pili ameahidi kuitunza kabisa mpaka afike kwako. Kisha? Simu inazimwa tena, unabaki ukilialia na kutusi kimoyomoyo.

Tukubaliane kwamba hakuna jinsia moja ambayo ni bingwa wa hadaa, zote mbili zimejaa matapeli na waongo wa kila aina.

Ndiyo maana wanaume wanalea watoto wasio wao wakidanganywa ni wao, kumbe kasaidiwa! Tutawaonea wanawake tukiwasingizia ujanja pekee.

Kisa na maana wanaume wengi wana nyumba ndogo kadhaa, tena kwa siri kuu. Panya wajanja mno, huuma na kupuliza!

Subiri hadi utakapofika muda wa dume kufukiwa kaburini uwaone wajukuu na vitukuu wakishuka mjini kutoka pembe zote za nchi, au hata dunia, kudai mirathi!

Visanga tele, hali mama mwenye nyumba wakati wote akidhani yuko peke yake, dume likiumwa analiuguza, likienda miayo analilisha, likililia chumbani analiliwaza na kutunza siri milele.

Kwa kifupi, mzaha wa ‘Baba’ kuwahusu Wakamba na wanawake kwa jumla ulikuwa hovyo, hakuufikiria kisawasawa kabla ya kuutoa. Kwa hivyo? Aha! Hamna kitu, tumemzoea.

Amenikumbusha miaka ya nyuma alipowakabili watu fulani waliodai asiyekutana na kisu cha ngariba hawezi kuchaguliwa rais.

Wakati huo aliuliza mwanamume anayezungumza kuhusu mtambo wa mwanamume mwenzake atakuwa ameuonea wapi ikiwa yeye si shoga!

Kisha? Mara moja akadai Rais George Bush wa Amerika na Waziri Mkuu Tony Blair wa Uingereza wakiongoza nchi zao vizuri hali hawakukatwa! Nilibaki nikijiuliza alijulia wapi!

 

[email protected]