Kinaya cha Kenya tajiri bila senti mifukoni

Kinaya cha Kenya tajiri bila senti mifukoni

CHARLES WASONGA na VICTOR RABALLA

MATATIZO ya kiuchumi yanayowakumba Wakenya yamewafanya wengi kuachwa na maswali ya ulipo utajiri ambao Rais Uhuru Kenyatta alidai umejaa nchini.

Akitoa hotuba bungeni mnamo Jumanne, Rais Kenyatta alisema chini ya utawala wake, utajiri wa nchi umeimarika kutoka Sh4.74 trilioni mnamo 2013 alipochukua madaraka kutoka kwa Mzee Mwai Kibaki hadi Sh11 trilioni sasa.

Rais Kenyatta alisema kutokana na utajiri wake mkubwa, Kenya sasa ni taifa nambari 6 tajiri zaidi barani Afrika ikilinganishwa na nafasi ya 12 mnamo 2013.

Lakini hali halisi ni umaskini wa kiwango cha juu miongoni mwa mamilioni ya wananchi, hivyo kufuta kauli ya Rais Kenyatta kwamba Kenya kuna utajiri mkubwa.

Baadhi ya wachanganuzi wanasema tatizo kubwa ni kuwa, kiwango kikubwa cha utajiri wa nchi kimo mikononi mwa watu wachache huku mamilioni wakibaki maskini hohehahe, hivyo kufanya utajiri alioangazia Kiongozi wa Taifa kukosa maana kwa wananchi wa kawaida.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya kiuchumi, ufanisi wa kiuchumi ambao Rais Kenyatta alieleza katika hotuba yake hauna manufaa yoyote kwa wananchi wa kawaida.

“Kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vile, mafuta, unga, sukari, mafuta ya kupikia, mkate, stima, gesi ya kupikia miongoni mwa mahitaji mengine kunaashiria maisha yamekuwa magumu kwa wananchi. Kwa hivyo, kiwango cha juu cha utajiri alichoeleza rais hakina maana yoyote kwao,” Bw Tony Watima, ambaye ni mwanauchumi, alisema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kwa mfano, kuanzia jana Jumatano, bei ya mkate wa uzani wa gramu 400 ilipanda kutoka Sh50 hadi Sh55.

Hii ni kutokana na kupanda kwa bei ya ngano inayoagizwa kutoka nje ya nchi, kwani kiwango kinachozalishwa nchini hakiwezi kukidhi mahitaji ya kitaifa.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), bei ya mafuta ya kupikia na gesi imepanda kwa hadi asilimia 30.

Kwa mfano, bei ya gesi ya kupikia ilipanda kuanzia Julai mwaka huu kwa asilimia 24.

Hii ni baada ya Wizara ya Fedha kuanza kutoza bidhaa hii ushuru wa ziada ya mapato (VAT) ya kiwango cha asilimia 16.

Hatua hiyo imepandisha bei ya kujaza mtungi wa kilo 13 wa gesi kutoka Sh2,019 hadi Sh2,503 jijini Nairobi.

Sababu kuu ya kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi, kulingana na Bw Watima, kunachangiwa na hatua ya serikali kupandisha viwango vya ushuru ili ipate fedha za kugharamia shughuli zake na kulipa madeni.

“Japo bajeti ya Kenya katika mwaka huu wa kifedha wa 2021/2022 ni Sh3.2 trilioni, mzigo wa madeni umefikia Sh8.3 trilioni. Hii ni sawa na asilimia 70 ya jumla ya utajiri wa Kenya ambao ni Sh11 trilioni,” akaongeza mtaalamu huyo.

Kulingana na Idara ya Bajeti Bungeni, mwaka huu, Kenya itaelekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika ulipaji wa madeni ya kigeni.

Hii kulingana na asasi hiyo, inaashiria kuwa serikali itaendelea kukopa ili kukimu mahitaji yake hata ingawa mamlaka ya KRA inakadiria kukusanya karibu Sh1.9 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Serikali ya Rais Kenyatta pia imeshindwa kukabiliana na athari za ukame ambao huathiri maeneo mbalimbali nchini kila mwaka, licha ya fedha nyingi kutengewa mipango ya kukabiliana na changamoto hiyo.

You can share this post!

Idadi ya wanaotumia ARVs yapanda kwa asilimia 83 –...

Obure ahusisha Mudavadi na kashfa ya Anglo-Leasing

T L