Kinaya cha UDA kuponda familia ya gavana Joho

Kinaya cha UDA kuponda familia ya gavana Joho

Na VALENTINE OBARA

UAMUZI wa Bw Mohamed Amir ambaye ni kaka ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho kujiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA), umekanganya kampeni za wanasiasa wanaoegemea chama hicho Pwani, hasa Kaunti ya Mombasa.

Bw Amir, ambaye ni mkubwa wa Bw Joho alijiunga na chama hicho alipohama ODM mwezi uliopita akipanga kuwania useneta Mombasa 2022.Wandani wa Naibu Rais William Ruto eneo la Pwani, hukashifu sana familia ya Gavana Joho kwa madai ya kuvuruga mandhari ya kibiashara Mombasa na uongozi duni wakati wa hatamu yake iliyoanza mwaka wa 2013.

Wakiongozwa na Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, na aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Omar Hassan, kampeni zao huwa hazikosi vijembe vikali dhidi ya familia ya Bw Joho.Mojawapo ya madai yao makuu ni kuwa familia ya Bw Joho imeteka biashara katika bandari ya Mombasa, na hivyo basi gavana huyo ameshindwa kutetea haki za Wapwani kufaidika na rasilimali hiyo kubwa.

Katika mikutano ya hadhara iliyoongozwa na Dkt Ruto tangu Jumamosi, wanasiasa hao waliendelea kukashifu biashara hizo za familia ya Bw Joho, licha ya kuwa Bw Amir alikuwa pamoja nao.Bw Ali alidai kuwa gavana huyo pamoja na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, walikuwa na uwezo wa kulinda maslahi ya Wapwani kunufaika na bandari hiyo lakini wakashindwa kufanya hivyo kwa sababu za kibinafsi.

‘2017 tuliahidiwa tutaenda Kanaani lakini badala yake wezi wakubwa wakachukua bandari yetu. Nilisimama katika Bunge la Taifa kutetea bandari lakini wabunge wenu wakasimama kunitusi. Bandari ya Pwani ikaenda…leo Mombasa imesalia mahame, hakuna lolote,’ akasema.

Katika hotuba ya awali, Bw Joho alitetea biashara za familia yake bandarini na kusema kandarasi zote ambazo kampuni yao ilipata kutoka kwa serikali zilikuwa halali.Kulingana naye, madai dhidi ya familia yake zina nia mbaya kwani kuna wafanyabiashara wengine wengi mashuhuri wakiwemo wanasiasa ambao pia hupata kandarasi katika Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) ilhali hawashutumiwi.

Familia ya Bw Joho huwa na kituo cha kuhifadhi na kusafirisha makasha ya mizigo inayoingia nchini kupitia bandarini.Biashara nyingi aina hiyo zilipata pigo wakati ilipoamuliwa mizigo inapowasili isafirishwe kwa reli mpya ya SGR hadi Nairobi, lakini kampuni chache zilibahatika kupata kandarasi katika KPA.

Kwa upande wake, Bw Hassan alidai kuwa iwapo Dkt Ruto ataunda serikali ijayo, viongozi wa Pwani wanaoegemea upande wake watahakikisha kuna mabadiliko kuhusu usimamizi wa shughuli katika bandari ya Mombasa ili wananchi wote wanufaike badala ya kunufaisha wafanyabiashara wachache.

“Tulibakishwa na rasilimali moja ya bandari lakini mpaka hiyo wakaichukua. Twataka kurejesha rasilimali yetu kubwa na rasilimali hiyo ni bandari. Sisi hatuna masilahi ya kibinafsi katika hiyo bandari wala SGR,’ akasema.Hata hivyo, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, aliyapima maneno yake kwa makini alipozungumzia suala hilo huku akitaka kumwepushia lawama Bw Amir kuhusu madai yanayoelekezwa kwa familia yake.

Bi Jumwa alidai kuwa, Bw Amir alionelea ni heri ajiunge na upande wa Dkt Ruto kwa vile hata yeye alikuwa hafaidiki na biashara wala ushawishi wa siasa wa familia yake.’Hii Mombasa Kaunti si ya familia moja. Hata hiyo familia inajipiga kifua eti wanadhibiti Mombasa, tuko na Amir Joho (amekaa) hapa nyuma.

Hata yeye hiyo familia haimsaidii ndipo akasema atatoka. Kama haimfaidi yeye, sembuse wewe Karisa na Katana,’ akadai.Katika mahojiano ya awali, Bw Amir alisisitiza kuwa uamuzi wake kujiunga na UDA haufai kuhusishwa na masuala yoyote ya familia yake.

You can share this post!

Familia kusherehekea Krismasi vichakani

2022: Mudavadi akataa Huduma Namba katika uchaguzi

T L