Makala

KINAYA: Huenda wakati umefika wa ‘Baba’ kusalitiwa na ‘Ouru'

September 22nd, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

ALA! Usiniambie ‘Baba’ amebebwa na maji ya mabwawa ya Kimwarer na Arror!

Vipi nawe ilhali mabwawa yenyewe hayakujengwa?

Tena, mwana wa Jaramogi kasukumwa na nani hadi mle ndani ndio atwaliwe na mawimbi makali hayo?

Wajua, kila kitu kinawezekana ndani ya Kenya hii yetu.

Wewe nami tunakubaliana kwamba mabwawa ya Kimwarer na Arror ni ya kufikirika sasa.

Naam, hasa! Hayakujengwa. Wanaume walitafuna pesa. Naye ‘Ouru’ ameifutilia mbali miradi hiyo, lakini akilini mwangu nayaona mawimbi makali.

Vipi nawe? Si huo ni wendawazimu? Unauliza. Nionyeshe yeyote ambaye hujishughulisha na siasa siku nenda siku rudi na bado ana akili timamu!

Kwa ufupi, mimi nawe tuna kasoro fulani. Haidhuru tukichunguzwa, lakini hadi itakapothibitishwa zimeruka, acha tujifurahishe hapa. Au sio? Kabisa yaani!

Basi kalia jamvi nikumegee niliyokuandalia, nikujuze ni kwa jinsi gani ambapo ninadhani ‘Baba’ ametwaliwa na mawimbi ya mabwawa ya kufikirika, yaliyo akilini mwetu tu.

Nimewahi kukuandikia hapa kwamba kabisa simwamini ‘Ouru’ kuhusu ule mkono wa maridhiano aliopokezana na ‘Baba’.

Mimi hudhani anampumbaza mzee wa watu.

Dalili za kutimia kwa utabiri wangu huo zilionekana juzi ‘Ouru’ alipofanya mambo mawili siku moja kwa mpigo!

Alifuta mradi wa Kimwarer kisha akampokea mwaniaji wa ubunge wa Kibra, mwanasoka McDonald Mariga, kwenye Ikulu ya Nairobi, na kuapa kumuunga mkono.

Hayo yanahusianaje? Rahisi sana. Si siri kwamba ‘Ouru’ na mdogo wake, Dkt Bill Samoei kutoka Sugoi, wamedhaniwa kutofautiana kuhusu mambo hayo mawili.

Unajua ‘Ouru’ ametukanwa si haba na domo-kaya wa Bonde la Ufa wakiongozwa na Seneta Murkomen tangu kashfa ya kuliwa kwa pesa za ujenzi wa mabwawa hayo ilipoibuka.

Waliotema matusi hayo, ambao ni marafiki wa Dkt Bill, waliichukulia kuwa hujuma hatua ya kuichunguza miradi hiyo, wakatabiri ingefutwa. Na imefutwa juzi, wakajiona manabii.

Vilevile, unajua marafiki wa ‘Ouru’ wanaojiita Kieleweke na wale wa ‘Baba’ katika ODM walivyomtukana Dkt Bill wakimwambia aisahau Ikulu kama alivyolisahau titi la mamake.

Kama nilivyotabiri, huenda wakati umefika wa ‘Baba’ kusalitiwa na ‘Ouru’, hasa baada ya kumtenganisha na washirika wake wa Nasa wanaomwona msaliti mkuu.

Kumbuka ni takriban miaka miwili kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu wa 2022, hivyo kwa ‘Ouru’ haidhuru mirengo ya siasa ikijitunga ili kuzichapa hadi hapo.

Kwa kufuta miradi na kumkumbatia Mariga, ‘Ouru’ amemkanganya ‘Baba’ hivi kwamba hajui amesalitiwa au amesaidiwa.

Mzee wa watu alitaka miradi ifutwe ili hasidi wake wa kisiasa, Dkt Bill, aaibike, na pia alitarajia Kibra iheshimiwe kama chumba chake cha kulala.

Najua unatarajia ‘Ouru’ atukanwe na wanamgambo wa ODM pamoja na wale wa Bonde la Ufa. Acha kuzubaa bwana, chemsha bongo!

ODM itaendelea kumtukana ‘Ouru’, nao waliofutiwa miradi wataagizwa na Dkt Bill wawatukane Man Giddy, mwana wa Mzee Kirungu, na ‘Baba’ badala ya ‘Ouru’.

Waliokanganyikiwa ni Kieleweke, hasa walioapa kutomuunga mkono Mariga. Hawajui wamwombe msamaha Dkt Bill au wajiunge na ODM. Siasa ni mbio za panya jangwani!

 

[email protected]