Makala

KINAYA: Kwani kuliendaje kwa 'Tangatanga' na ODM baada ya BBI kutolewa?

December 1st, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KWA nini naona kama ‘Baba’ amechezewa shere?

Ripoti ya BBI iliyotolewa juzi haijamkalia vizuri, ndiyo maana ameanza kulalamika.

Hata domokaya Atwoli amesema ripoti hiyo ikitekelezwa ilivyo nchi hii itagawanyika kuliko mwanzo.

Atwoli anajulikana kumtetea ‘Baba’ na kuchukua misimamo yake kikweli.

Kwani kuliendaje ilhali kabla ya Jumatano iliyopita, ripoti hiyo ilipozinduliwa, ‘Baba’ na watu wake waliunga mkono BBI huku timu ya ‘Tangatanga’ ikitishia kususia mchuano huo?

Hata wasiri wakuu wa ‘baba’ wanajua fika kwamba kuna mambo yaliyokwenda kinyume na matarajio yao, lakini hawataki kutamka hili wazi wasimkasirishe mwenyeji wa Ikulu.

Kwa nini wasimkasirishe? Wanaamini ni mshirika wao wa kisiasa wakati huu, ambaye ana uwezo wa kumpiga chenga Dkt Bill Samoei na kumkabidhi ‘Baba’ Ikulu.

Wala asikwambie mtu! Utakuwa zuzu wa kupigiwa mfano ukiamini harakati zote za ‘Ouru’ na ‘Baba’ ni kwa manufaa yako Mkenya wa kawaida au nchi nzima kwa jumla.

Mkakati mkuu hapa ni kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 na zaidi.

Hata mkuu wa ‘Tangatanga’, Dkt Samoei, anateta mchana kutwa kwa sababu iyo hiyo.

Hali ikiwa hiyo, kila mdau anajua kwamba akipepesa jicho tu, atapigwa ngware na kujipata chini!

Binafsi sijali atakayebwagwa ni nani, bora watuachie nchi salama.

Najua Wakenya wengi wamekanganyikiwa wakati huu, hawana hakika dai la ‘Tangatanga’ kuiunga mkono ripoti hiyo ni la kweli. Wanadhani ni ule ujanja wao wa kawaida.

Lakini, hata ingekuwa wewe, ungewaamini ‘Tangatanga’ vipi ilhali juzi walipobwagwa katika Uchaguzi Mdogo wa Kibra walitanua vifua na kudai walipiga hatua muhimu?

Si tangu jadi mchezo huu wa siasa, cha muhimu huwa ni wingi wa kura? Si hata katika kabumbu kulisha watu chenga huwa bure ikiwa hamna mabao? Acheni mzaha.

Ijapokuwa ni watu wachache sana wanaoweza kuliamini kundi la ‘Tangatanga’, eti sasa linaunga mkono Ripoti ya BBI kwa sababu inalifaa, nadhani kuna ukweli fulani.

Sasa ‘Baba’ anaambia watu nini kuhusu Ripoti hiyo, hasa kutokana na ukweli kwamba wadhifa wa Waziri Mkuu anaonasibishwa nao hauna mamlaka yoyote?

Anaambia watu nini ikiwa akitaka kuwa Waziri Mkuu ni lazima kwanza awanie na ashinde ubunge kisha ateuliwe Waziri Mkuu kwa hisani ya yeyote atakayekuwa Rais?

Anaambia watu nini ikiwa hapo 2022 ni sharti azichape na mkuu wa ‘Tangatanga’, Dkt Samoei, akishindwa atulize boli mpaka 2027 ili kujaribisha bahati tena?

Pendekezo la washirika wa ‘Baba’ kwamba kuteuliwe jopo la wataalamu ili waihariri na kuinyoosha Ripoti ya BBI kabla haijapigiwa kura ya maamuzi ni zuri. Hatuwezi kuwaaminia wabunge jukumu kubwa kama la kuibadili Katiba.

Hata hivyo, kumbuka kuna kongamano kuu la Katiba ambalo linatarajiwa kufanyika Januari mwakani. Je, wajanja wa ‘Tangatanga’ wakiamua kuchelewesha shughuli hizo hadi baada ya 2022?

Ukitaka usiniamini, lakini nimesema hapa na kurudia mara kadha kwamba bado nadhani kuna uwezekano kwamba ‘Ouru’ anamcheza shere ‘Baba’.

Ikiwa sivyo, iweje mapendekezo yote ya Dkt Samoei yamo kwenye BBI na ya ‘Baba’ ni kuonjeshwa tu?

 

[email protected]