Makala

Kinaya mafuriko yakitatiza jiji licha ya mikakati kuzuia athari

March 31st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MNAMO Septemba mwaka uliopita, Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi alizindua mipango kabambe ya kulitayarisha jiji dhidi ya athari ambazo zingetokana na mvua ya El-Nino.

Idara ya Kutabiri Hali ya Hewa Kenya (KMD) ilikuwa imetangaza kuwa mvua hiyo ingenyesha kati ya Septemba 2023 na Januari mwaka huu, 2024.

Kama njia ya kujitayarisha mapema dhidi ya athari hizo, Kaunti ya Nairobi—sawa na kaunti nyingine nchini—zilianza mipango kabambe kujitayarisha dhidi ya madhara yoyote ambayo yangesababishwa na mvua.

Mikakati hiyo ya matayarisho ilikuwa ikiongozwa na Gavana Sakaja mwenyewe.

Baadhi ya mikakati hiyo ilihusisha kuhakikisha mitaro yote ya kusambaza majitaka jijini na viungani mwake haijazibwa kutokana na mrundiko wa taka.

Kaunti pia ilianza mikakati ya kuziba mashimo katika baadhi ya barabara inazosimamia.

“Lengo kuu la kaunti ni kuhakikisha kwamba tunalinda wakazi dhidi ya athari za mafuriko. Hatua ya kwanza ambayo tumehakikisha ni kufungua mitaro yote kusambaza majitaka katika kila sehemu. Pili, tumeajiri maafisa maalum 3,500 wa mazingira ili kutusaidia kwenye zoezi hilo,” akasema.

Zaidi ya hayo, Bw Sakaja aliiagiza Idara ya Kusimamia Ujenzi ya Kaunti kubaini maeneo salama ambako wakazi wangehamishiwa ikiwa makazi yao yatakumbwa na mafuriko.

Gavana pia alitangaza kwamba kaunti ilikuwa imenunua malori mapya, ambulensi na magari mengine ya kutumika, ikiwa kuna hali zozote za dharura zitakazotokea wakati wa mafuriko.

Ingawa wakazi wengi jijini walitarajia mikakati iliyokuwa imewekwa na kaunti ingezaa matunda, wengi wanalalama kuwa hali ni ile ile ambayo imekuwepo miaka nenda miaka rudi, mvua inaponyesha.

Mnamo Machi 24, 2024, watu saba waliripotiwa kufariki katika maeneo tofauti jijini kutokana na athari za mvua kubwa iliyonyesha nyakati za usiku.

Mvua hiyo kubwa pia ilisababisha uharibifu mkubwa katika sehemu tofauti jijini.

Miongoni mwa wale waliofariki ni polisi aliyekuwa akijaribu kuokoa watu dhidi ya athari za mafuriko hayo.

Kulingana na Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Adamson Bungei, polisi huyo alikuwa akielekea katika steji ya magari ya Country Bus kuokoa watu wanne waliokuwa wamekwama kutokana na mafuriko hayo.

Katika mtaa wa Dandora Phase 5, familia moja iliachwa katika hali ya majonzi baada ya msichana wao kusombwa na mafuriko alipokuwa akijaribu kuvuka daraja moja karibu na Mto Nairobi.

Kisa hicho kilifanyika wakati wanafunzi wawili –akiwemo msichana huyo-walikuwa wakijaribu kuvuka daraja hilo kuelekea katika Shule ya Msingi ya Ushirika.

Mitaa mingine ambako wakazi wamelalama kuathiriwa na mafuriko ni Mukuru Kwa Njenga na Mukuru kwa Reuben.

Wenyeji wa mitaa hiyo wanasema kuwa wakati umefika kaunti ihakikishe kuwa miundomsingi iliyowekwa kudhibiti mafuriko inafanya kazi.

“Miundomsingi mingi iliyopo, kwa mfano madaraja, haina uthabiti wa kutosha kuhimili nguvu za maji wakati mafuriko yanapotokea,” akasema Bw James Kioko, ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mukuru kwa Njenga, kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.