Makala

KINAYA: Mariga hana deni lako, huwezi kumlazimisha kufanya hisani

September 8th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI wewe kabwela mzee una nini?

Mbona unamchukia mtoto ilhali unaitwa baba? Watoto wako wakichukiwa utahisije?

Samahani, siutukani uzee ila lazima niujadili hapa, katika muktadha wa udaku wa kisiasa unaoendelea Kenya.

Wazee fulani wanaungulika wakiona vijana wakijitosa ulingoni kuzichapa kisiasa. Watakereketwa sana!

Na wakishindwa wameze nyembe; kwenye siasa hakuna kiti cha mtu, sote tunatafuta. Asiyeangukiwa na bahati aridhike, siku yake itafika na isipofika, basi ole wake.

Siasa za Kenya zina mambo eti. Na wajuaji kibao, wengi wa kiherehere na upungufu wa maarifa. Watazuka waropokwe na maneno kabla ya kuyatafakari, tafakuri ni baadaye eti.

Juzi nimemkabili mjuaji fulani alipozuka kwa fujo kumtaka mwanasoka McDonald Mariga, kabla ya kuingia siasa, atangaze ametumia pesa zake vipi kuifaa jamii.

Hebu tazama kinaya hapa: Kabwela aliyedai maelezo ana umri wa miaka 45 ilhali Mariga ana 32 pekee.

Wala kabwela hana haya akilalamika kwamba hajanyeshewa na neema za Mariga na sifa zote za kucheza kabumbu ya kulipwa.

Nilimuuliza yeye mwenyewe, kwa kuwa amemzidi Mariga kwa umri, alimsaidiaje kufikia upeo wa juu wa soka kutoka mazingira magumu aliyokulia kijana huyo.

Kabwela aliuma mdomo wa chini, akauacha na kuuma wa juu, kisha akasema Mariga ana pesa nyingi kumzidi hivyo basi anapaswa kuwa amemsaidia kwa kiasi fulani.

Nilishikilia kwamba yeye na umri wake mkubwa anapaswa kuwa mlezi na wala si mtegemezi wa kijana huyo.

Niliachana na kabwela huyo nilipoona fikra zake duni za kutaka kusaidiwa haziwezi kubadilika kamwe.

Si ajabu mtoto amempiku kwa kila kitu, mpaka kutamani kuwa mbunge mpya wa Kibra ifikapo Novemba 7, naye kabwela anashiriki umbea tu. Kuna wengi sampuli hiyo.

Ni unafiki kwa watu kuanza kuuliza Mariga – ambaye anatarajiwa kubeba mwenge wa chama cha Jubilee katika kinyang’anyiro hicho – ameisaidia jamii namna gani.

Ni hujuma kumtarajia mtu kutumia mshahara wake binafsi kuisaidia jamii. Hakuna anayepaswa kulazimishwa kutenda hisani kabisa.

Hata walafi tunaoita wabunge hawatumii mishahara yao binafsi, wametengewa mfuko wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Kwa mtu mzima na ndevu zake, nikidhani anaitwa baba, kumtarajia mdogo wake kwa miaka zaidi ya 10 kuwa mkombozi wake kiuchumi ni kasumba ya kimaskini sana. Ikome!

Kujituma

Kila mtu anapaswa kujituma kivyake kuchuma anachoweza, si kutegemea cha nduguye. Vitabu vitakatifu vinaniambia asiyefanya kazi na asile.

Nguvu nyingi wanazotumia makabwela kulalamika kwamba fulani hajawafaa kwa chochote zinapaswa kutumika katika shughuli za kuzumbua riziki, si kushiriki umbea.

Kwa kuwa mwanasoka wa kwanza kutoka Kenya kusakata kabumbu kwenye ligi ya UEFA, Mariga amewashawishi vijana kiakili wakajua wanaweza kufika mbali pia.

Kina pangu pakavu tia mchuzi watakula huu na hasara juu! Huu ni ulimwengu wa kibepari ambapo unachuma kivyako na kula kivyako; mtegemea cha nduguye afe maskini!

Kwa vyovyote vile, kinyang’anyiro cha Kibra kitakuwa cha kupendeza sana kwani tutawashuhudia ‘Baba’ na Dkt Bill Samoei wakiraruliana magwanda hadharani. Usikose!

 

[email protected]