Makala

Kinaya Mlima Kenya kupasuka Rais Kenyatta akistaafu

November 15th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

ANAPOJITAYARISHA kung’atuka uongozini mwaka 2022, Rais Uhuru Kenyatta anaandamwa na kinaya cha kuzua mgawanyiko kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya anapojaribu kuwauzia wenyeji ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Hii ni kinyume na ilivyokuwa mwaka 2013, ambapo wenyeji waliungana pamoja kumchagua kama Rais pamoja na Naibu Rais William Ruto, kutokana na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu yaliyowakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa za Mlima Kenya, huenda Rais Kenyatta pia akawa kiongozi wa kwanza katika eneo hilo kustaafu urais akiliacha eneo hilo likiwa limegawanyika kisiasa.

Hata hivyo, hilo litadhihirika tu ikiwa Rais atashindwa kuyaunganisha makundi pinzani ya kisiasa ambayo yameibuka kufuatia mdahalo unaoendelea kuihusu ripoti hiyo.

Kulingana na wakili Ndegwa Njiru, ambaye ni mdadisi wa siasa, imefikia wakati Bw Kenyatta atazame ‘nyayo’ za watangulizi wake kama Mzee Jomo Kenyatta na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, ambao walijaribu kufanya kila wawezalo kuzima migawanyiko ya kisiasa iliyokuwepo kati ya jamii za GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru).

“Ingawa Rais Kenyatta ana lengo nzuri kuiunganisha nchi kupitia BBI, lazima pia atazame mwelekeo wa kisiasa katika ngome yake, ili asije akayaunganisha maeneo mengine na kusahau nyumbani,” asema mchanganuzi huyo.

Eneo hilo limejipata kama ‘mateka’ wa makundi pinzani kisiasa; Kieleweke na Tangatanga, moja likidai ‘kumtetea’ Rais Kenyatta huku lingine likimuunga mkono Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuna hatari kubwa siasa za BBI kufufua upya uhasama wa kisiasa kati ya makundi hayo mawili na kufifisha kabisa nafasi ya Rais Kenyatta kurejesha umoja wa kisiasa uliokuwepo awali.

Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Tangatanga wanasema ripoti hiyo ilipuuzilia mbali maslahi ya wakulima ambayo wamekuwa wakiyatetea kama kuboreshwa kwa bei za kahawa, majanichai na ufugaji, ambazo ndivyo vitegauchumi vya idadi kubwa ya wenyeji ukanda huo.

Baadhi ya wabunge hao ni Rigathi Gachagua (Mathira), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu) kati ya wengine.Kwa mujibu wa Bw Gachagua, kundi hilo liko tayari kuwarai wananchi kuiangusha ripoti hiyo, ikiwa haitajumuisha matakwa ya wakulima.

“Tunafahamu kwamba huu ni mradi wa Rais Kenyatta, ambao lengo lake kuu ni kuleta umoja nchini. Hata hivyo, hatutakubali hali ambapo maslahi ya wafuasi wetu yatapuuzwa kwa kisingizio cha kuleta umoja,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo pia alisisitiza nia yao si kutomheshimu Rais, bali wao ni ‘sauti’ ya mamilioni ya watu ambao wanahisi kutengwa na utawala wa Rais Kenyatta.

“Ni lazima Rais Kenyatta aangalie nyuma na kubaini sababu ya migawanyiko kuzuka ‘nyumbani’ kwake, licha ya juhudi za kuiunganisha nchi. Mbona ngome yake imegawanyika kinyume na ilivyokuwa wakati alichaguliwa kama Rais mnamo 2013? Kuna hatari akavuruga umoja uliokuwepo anapostaafu,” akasema Bw Gachagua.

Haya hivyo, wanasiasa wa kundi la Kieleweke wanamtetea vikali Rais Kenyatta, wakisema kuwa lengo la wenzao katika Tangatanga ni kumsawiri kama kiongozi “asiyejali maslahi ya wenyeji wa Mlima Kenya.”Wanasema hiyo ndiyo mbinu wanayolenga kutumia ili “kumfanyia kampeni Dkt Ruto” katika ukanda huo.

“Tunafahamu kwamba lengo kuu la Tangatanga ni kumharibia sifa Rais Kenyatta kwa kuwagawanya wenyeji wa Mlima Kenya. Ni sababu hiyo ambapo Dkt Ruto amekuwa akifanya kampeni za kuipinga BBI katika eneo hilo pekee,” asema mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, ambaye ni miongoni mwa wakosoaji wakuu wa Dkt Ruto.

Baadhi ya wazee katika Baraza la Kitaifa la Agikuyu (KCE) wanasema kuna haja ya viongozi wa kidini, kitamaduni, mabwanyenye na watu maarufu eneo hilo kufanya kikao cha pamoja ili kutathmini kiini cha migawanyiko iliyopo.

Kulingana na Askofu Lawi Imathiu, ambaye ni miongoni mwa wasimamizi wakuu wa Chama cha Kitamaduni cha Jamii za Gema (GCA), mjadala kama huo ndio njia pekee itakayohakikisha ukanda huo umedumisha umoja, hasa nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Anasema ni kinaya ukanda huo kukumbwa na migawanyiko, kinyume na ilivyokuwepo katika miaka ya sitini, sabini na themanini.Anaeleza kuwa wakati huo, wanasiasa kama marehemu Njenga Karume, Kenneth Matiba, Kihika Kimani, Mbiyu Koinange kati ya wengine walikuwa nguzo kuu zilizounganisha ukanda huo.

“Wanasiasa hao pia walitoa ushauri muhimu kwa Mzee Kenyatta na viongozi wengine kuhusu umuhimu wa kuzingatia umoja. Msingi huo ulidhihirika hata wakati marehemu Daniel Moi alipojaribu kulivuruga kisiasa. Wenyeji walidumisha umoja kwa miaka 24 ambapo Bw Moi alikuwa uongozini,” asema Askofu Imathiu, akisema umoja huo ulitokana na mbegu ya mshikamano iliyopandwa na Mzee Kenyatta.

Vivyo hivyo, anasema Rais Kenyatta anapaswa kufuata nyayo za babake, kwa kuhakikisha anayaunganisha makundi yote pinzani anapojitayarisha kustaafu. Hata hivyo, wakosoaji wa Rais wanamtaja kama “baba aliyesahau nyumbani” hivyo itakuwa vigumu kurejesha umoja uliokuwepo.