MakalaSiasa

KINAYA: Naona ni heri tuiuze Kenya kila mtu agawiwe hela arudi kwao

February 11th, 2018 2 min read

Wakili mbishi na mwanasiasa wa NASA aliyefurushwa kutoka humu nchini na kurudishwa nchini Canada, Dkt Miguna Miguna. Picha/ Maktaba

Na DOUGLAS MUTUA

Kwa Muhtasari:

  • Ikiwa huna kwenu kwingine, anza kuuliza wazee wako mlitoka wapi kabla ya kuja Kenya
  • Hapa ndipo siasa za uapisho na uhamiaji zilipotufikisha. Nikizingatia hali hii, naona Kisiwa cha Migingo kikikabidhiwa Uganda rasmi
  • Mashtaka atakayofungua Miguna, ikiwa tayari hajayafungua, yatakushangaza

KENYA ni ya nani? Nauliza tu kwa sababu yumkini kuna watu walio na hatimiliki ya nchi hii – kama ya shamba au ploti hivi – wanaoweza kukwambia ufunganye.

Ikiwa huna kwenu kwingine, anza kuuliza wazee wako mlitoka wapi kabla ya kuja Kenya kwa maana hakuna hakika huku kutasalia kwetu daima.

Binafsi sina wasiwasi; walikotoka mababu wa mababu zangu, ndani ya misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kungalipo, tena hakujalimwa na yeyote.

Nahitaji tu kumsadikisha Rais Joseph Kabila kwamba haja yangu ni pahali pa kuita nyumbani, aniruhusu nipenyeze hadi katikati ya msitu na kujenga msonge wa Kikamba.

Nitaukandika kwa udongo na kuuezeka kwa nyasi, nile matunda na mizizi ya porini kabla ya kuanza shughuli za kilimo, niendelee na maisha yangu mbali na usumbufu wa serikali.

Hapo ndipo siasa za uapisho na uhamiaji zilipotufikisha. Nikizingatia hali hii, naona Kisiwa cha Migingo kikikabidhiwa Uganda rasmi, Wakenya fulani waambiwe wahamie huko na wasiote wakirudi Kenya.

Lakini Migingo ni ndogo sana, umati wa watu nilioona katika Bustani ya Uhuru Park wakati wa sarakasi ya uapisho wa ‘Baba’ hawawezi kutoshea hapo.

 

Kurudi Nigeria

Ikiwa watu wanarudishwa kunakodhaniwa kwao, hata kama hawataki, nitawashauri wafuasi wa ‘Baba’ wajiandae kuvuka mpaka kuingia Sudan, njiani kurudi Nigeria.

Kila mtu akirejeshwa kwao, tutaona mrejeshaji watu atakalia nani kimabavu. Ni uraibu wa binadamu wakati wote kuwa na mtumwa wa aina fulani.

Nimesema mara nyingi hapa kwamba nakubaliana na wachekeshaji wanaopendekeza tuuze Kenya, tugawane hela kila mtu atie zake kibindoni na kujiondokea.

Ikiwa tunachukiana kiasi cha kutoweza kuishi pamoja kwa amani wala kujitawala, ikizingatiwa kwamba Kenya si ya mama wa mtu, mbona tusiigeuze pesa na kuzigawana?

 

Sote tuko sawa

Nasema hivi kwa sababu naamini kwa dhati ya moyo wangu kwamba hakuna Mkenya bora kuliko mwingine, sote tuko sawa machoni pa Mwenyezi Mungu na Katiba.

Unapotoka pale unaponitishia eti kwa sababu nina nyumba Marekani, Canada, Uingereza, Tanzania au Uganda, unajiona bora kunizidi katika ushirika huu uitwao Kenya.

Nakumbuka nikiijadili Katiba ya sasa na mwendazake Mutula Kilonzo, aliyekuwa waziri wa masuala ya kikatiba, muda mfupi baada ya sheria hiyo kuu kupitishwa.

Alinihakikishia kuwa niko radhi iwapo ningetaka kuhama Kenya kuishi nchi za watu kwa maana hakuna anayeweza kunipokonya haki ya uzawa!

Katiba yenyewe inanihakikishia haki hiyo, hivyo kondo langu la nyuma lililozikwa Kenya nilipotoka tumboni mwa mama haliwezi kufukuliwa likaletwa Marekani ninakoishi; Kenya ni kwetu.

Bila shaka umejionea ya Miguna, yule bwana anayetumia jina moja mara mbili.

 

Mshangao unakusubiri

Nisikize kwa makini: mashtaka atakayofungua Miguna, ikiwa tayari hajayafungua, yatakushangaza.

Atatushtaki sote, waliotaka ahamishiwe Canada na waliomtaka asalie Kenya kama ‘jenerali’ wao, hata wahudumu ndani ya ndege, sikwambii hata Malkia wa Uingereza atashtakiwa kwa maana ndiye mkuu wa Jumuiya ya Madola!

Polisi watatakikana kueleza vilikokwenda viatu vyake, akalazimika kuingia ndani ya ndege na champali za kwendea msalani.

Nitakukariria alivyopenda kusema Jakaya Mrisho Kikwete enzi zake akilala Ikulu ya Tanzania pindi maji yalipokaribia kuzidi unga: “Upepo utapita tu.”