Makala

KINAYA: Ngilu anawazibia Wakambodia soko la matikitimaji na maembe

March 4th, 2018 2 min read

Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu. Amepiga marufuku biashara ya makaa katika kaunti yake. Picha/ Maktaba

Na DOUGLAS MUTUA

MAMA Mwenge na kiherehere chake cha kuchoma magari ya watu yanayosafirisha makaa asipodhibitiwa, Wakamba hatutaweza kuuza ‘watermelon’ zetu ‘ng’ambo’.

Hicho ndicho kichekesho bora zaidi nilichosikia wiki iliyopita kutoka kwa Mkambodia fulani wa Kitui asiyempenda Wiper, yule bwana aliyepewa msimbo wa tunda la tikitimaji.

Kichekesho chenyewe kilikuwa kama utabiri kwa maana ghafla bin vuu magari ya watu yalianza kupasuliwa magurudumu na kutolewa pumzi na wehu wa Kiambu ya ‘Baba Yao’.

Hata kabla ya mbavu kuacha kuniuma, kichekesho kingine kilitokea karibu mlimani Kenya kikiwaambia Wakambodia waheshimu wauzaji makaa, maembe ni ya msimu.

Kwa nini maembe? Kutokana na ukavu wa Ukambani, matunda bora kama maembe, matikitimaji, machungwa na kadhalika hutoka huko.

Dhamira ya kichekesho cha pili ni kutukumbusha sote kwamba, japo tuna tofauti zetu za kikabila na kimapato, tunahitajiana kwa njia moja au nyingine. Hakuna wanaojitosheleza.

Tunategemeana katika nyanja zote: siasa, uchumi na jamii. Mkenya bora ni anayejaribu kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anapata ufuasi kitaifa akitaka kuwa chochote.

Ni kwa mintaarafu hii ambapo nashikilia kuwa ukichonganisha watu kikabila kama ‘Mama Mwenge’, au ukimbie uapisho na kuaibika kimataifa kama ‘Watermelon’, hupati kitu!

 

‘Tikitimaji mtu’

Sina shaka nikisema matikitimaji ya Wakambodia huenda ndiyo bora zaidi nchini, wala sina shaka yanauzika kimataifa, ila ‘tikitimaji mtu’ wa Tseikuru hauziki kokote!

Ndiyo sababu unasikia msisitizo kwamba “chama ni ODM!” Watu wamechoshwa na uhafifu wa Wiper, hasa tangu alipomwacha ‘Baba’ kwenye mataa siku ya uapisho.

Hawataki kusikia eti kulikuwa na makubaliano kwamba ‘Baba’ amuunge mkono Wiper ifikapo 2022, eti hilo ni deni ghali mno kulipika. Ni sawa na kuuza nchi utumwani!

Sasa wafuasi wa ODM wanamtaka ‘Sultan Mwitu’ wa Mombasa avaane mzimamzima na Bill Kipchirchir Samaoei katika kinyang’anyiro hicho, na ‘Sultan’ mwenyewe habishi.

Kwa huhofia mchuzi kumdondoka kutoka kinywani, ‘Bwana Tikitimaji’ amejitokeza kukanusha madai yote ya uoga dhidi yake, akatahadharisha vijembe vitaleta utengano.

Mwingereza atakwambia uvumi husalia uvumi tu hadi utakapokanushwa; mtu anapokwambia kwamba yeye si tikitimaji, jua anaukiri utikitimaji!

 

Mchuano mkali

Binafsi ni miongoni mwa Wakenya wanaouchangamkia sana uwezekano wa mchuano kati ya Bill Samoei na ‘Sultan Mwitu’ hapo 2022. Simtaki Wiper, MaDVD wala Weta.

Natamani kinyang’anyiro kati ya Bill na ‘Sultan’ kwa maana wote wakali wa kutoa maneno mazitomazito, si waoga kama ‘Wiper’, wana mafedha chungu mbovu, tena hawajakonga.

Nani kakonga kwani? Atakuuliza Mkambodia anayemshabikia Wiper. Usimjali, kwao hawazeeki, ndiyo maana wengi wamesubiri kwa miaka zaidi ya 30 Wiper awe rais.

Kwao somo wangu Dkt Alfred Nganga Mutua, yule kijana wa sinema kutoka Jimbo la Masaku, angali mtoto.

Tafakari Bill na ‘Sultan’ wakizichapa, ujiulize ndimi zao kali zitatoa maneno yapi! Tafakari ‘Baba’ akimuunga mkono ‘Sultan’; ‘Ithe wa Jaba’ Samoei. Kampeni ya kukata na shoka!

Bill na ‘Sultan’ wakigawana vijana wakali kisiasa wanaowaunga mkono sasa, wazee kama Wiper na MaDVD hawatakuwa na lao ila kufunganya, nasi tutafaidi burudani kabambe. Naitamani siku hiyo.
[email protected]
JE, WAJUA?
Wanyama wote ni sawa, ila baadhi yao ni sawa kuliko wengine? Ungekaidi amri ya kufungua gari ili ukamatwe kama alivyofanya Jimi Wanjigi juzi, gari lingeguzwa kichujio kwa risasi, nawe mnofu!