Makala

KINAYA: Nilikuwa na hisia kwamba Haji, Kinoti wangeanza kuhasimiana

March 8th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

ALA! Kumbe wahenga hawakutupaka mafuta kwa mgongo wa chupa walipolafudhi kwamba fahali wawili hawakai zizi moja!

Nilijua kitambo! Hivi kujua nini? Kwamba udugu wa Noordin Haji na Kinoti ni wa muda, yaani kama biashara ambapo muamala ukifikia mwisho kila mtu huchanganya nyayo kwenda zake.

Sasa nasikia Bw Haji, yule mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) ambaye nyakati fulani huzungumza kwa ukali bila kupepesa macho, amekalia faili za watu.

Watu gani hao? Eti mafisadi ambao Kinoti, yule mkurugenzi wa upelelezi wa jinai (DCI) anataka washtakiwe, ikibidi wafungwe na kuozea jela.

Hivi kati ya Haji na Kinoti, nani mkuu?

Sheria ilivyo ni kwamba Haji ana usemi, kwa maana ndiye anayeamua ushtakiwe au uachwe kwanza uive kwa uhalifu.

Kinoti naye? Eti kazi yake kutuma mapendekezo tu kwa Haji, kwamba mshtaki huyu na huyo, yule sina hakika naye.

Na akishapendekeza? Eti asubiri ataitwa, aambiwe aendelee na safari ya kuwafikisha mahabusu mahakamani au kajaribu tena.

Kisa na maana? Idara ya DCI haina mawakili wake, kazi ya kuwafungulia watu mashtaka na kuwatoa kijasho chembamba mahakamani ni ya ofisi ya Haji.

Sasa nina hakika unajua mkuu kati ya hao ni nani. Ni sawa na timu mbili maarufu mno za soka – Manchester United na Arsenal – kubishania umaarufu ilhali mashabiki wanajua sogora ni nani.

Hata akiwa mkali kiasi gani, Kinoti hawezi kumshurutisha Haji kufanya kazi kwa namna fulani. Ni sawa na kumwelekeza fundi wa mashtaka jinsi ya kufanya kazi yake.

Najua bila shaka umewahi kusikia mtu akiulizwa: unataka kunifundisha kazi yangu? Si swali zuri, aghalabu huwa tishio kwamba mtu apeleke kiherehere huko mbali.

Hivi kwa nini Kinoti anadhani kwamba anaweza kumshinikiza Haji kufanya chochote? Sidhani anadhani hivyo, anajieleza tu kama binadamu yeyote anayejiona mkali.

Lakini kumbuka tangu hapo makali ya kisu na wembe yana tofauti, hasa ikiwa vifaa vyote viwili vitakabiliana. Itabidi kimoja kiwe butu ili amani ipatikane.

Nimekwambia nilijua wawili hao wangeanza kuhasimiana; wote ni watu na misimamo mikali, wachapa kazi sawasawa, sampuli ya watu ambao Kenya inahitaji.

Hata hivyo, kawaida ya binadamu akijua madaraka aliyo nayo hujaribu kuyadhibiti na kuyatumia atakavyo ili kuwakumbusha washindani kwamba wakithubutu watakomeshwa.

Historia ya Kinoti tunaijua: Ni ofisa mkali wa polisi, tena shupavu aliyewahi kuponea chupuchupu baada ya kumiminiwa risasi na wezi wa mabavu wakamwacha wakidhani kafa.

Kisa chenyewe kilifanyika eneo la Ruaraka, Nairobi, na naambiwa risasi alizofumwa zilimpasua utumbo ukaanguka chini, miguu na mikono ikavunjwa, lakini siku yake ilikuwa bado.

Kwamba aliipita mitihani hiyo yote ya kimaisha, akapanda vyeo hadi kuwa mkuu wa makachero nchini ni hali inayompa hisia kwamba hapaswi kudhibitiwa na yeyote.

Haji naye ni nani? Kabla ya kuanza kuwashtaki wahalifu kama DPP, mwana huyu wa Seneta Yusuf Haji wa Garissa alikuwa naibu mkurugenzi wa shirika la ujasusi nchini (NIS).

Aliwanasa washukiwa wengi wa ugaidi na kuwapeleka Uganda ambako walifungwa maisha, sikwambii wapiganaji wa al-Shabaab wanasaka kichwa chake. Na hajali.

Mwamuzi wa fahali hao wawili ni aliyewapa kazi.

 

[email protected]